Mgonjwa akizukiwa na maradhi katikati ya Ramadhaan na yeye amefunga na akapata uzito wa kuikamilisha basi itafaa kwake kufungua kwa sababu kuna sababu inayomruhusu kufanya hivo. Akipona mchana wa Ramadhaan na yeye ni mwenye kula basi haitosihi kufunga siku hiyo kwa sababu alikuwa ni mwenye kula sehemu ya mwanzo ya mchana. Swawm ya lazima haisihi isipokuwa kuanzia kuchomoza kwa alfajiri. Je, ni lazima kwake kujizuia masaa yaliyobaki ya siku hiyo? Wanachuoni wametofautiana, jambo ambalo tumekwishatangulia kulitaja kuhusu msafiri akifika katika mji wake hali ya kuwa hakufunga.

Ikithibiti kimatibabu kwamba kufunga kunamletea maradhi au kunamcheleweshea yeye kupona basi itafaa kwake kuacha kufunga kwa sababu ya kuchunga afya na ugonjwa wake. Ikiwa khatari hii inatarajiwa kuondoka basi atasubiri mpaka iondoke. Baada ya hapo atalipa zile siku alizokula. Ikiwa maradhi hayo hayatarajiwi kuondoka basi hukumu yake ni ileile ya fungu la tano ambapo atakula na atalisha chakula kumpa maskini kwa kila siku moja iliyompita.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 53-54
  • Imechapishwa: 06/05/2020