Swali 38: Unasemaje juu ya yale wanayoonelea baadhi ya watu kwamba du´aa ya kukhitimisha Qur-aan ni miongoni mwa Bid´ah zilizozuliwa?

Jibu: Sijui du´aa ya kukhitimisha Qur-aan ndani ya swalah msingi sahihi ambao kwao mtu anaweza kutegemea juu yake kutoka katika Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala kutoka katika matendo ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Kubwa linalopatikana katika hayo ni yale yaliyokuwa yakifanywa na Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) anapotaka kumaliza Qur-aan basi alikuwa akiwakusanya familia yake na akiomba du´aa. Lakini hata hivyo alikuwa hafanyi hivo ndani ya swalah yake. Swalah, kama inavyofahamika, ni jambo halikuwekwa katika Shari´ah kuzusha du´aa maeneo ambayo hapakupokelewa Sunnah juu yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalini kama mlivyoniona nikiswali.”[1]

Ama kusema kwa kuachia kwamba ukhitimishaji huu wa ndani ya swalah ni Bid´ah mimi sipendi kusema hivo moja kwa moja kwa kuachia. Kwa sababu wanachuoni wa Sunnah wametofautiana juu ya jambo hilo. Kwa hivyo hatutakiwi kuchupa mpaka kiasi hichi juu ya jambo lililosemwa na baadhi ya wanachuoni wa Ahl-us-Sunnah ya kwamba ni miongoni mwa mambo yaliyopendekezwa. Lakini lililo bora kwa mtu ni yeye awe mwenye pupa juu ya kufuata Sunnah.

Kwa kuongezea ni kwamba hapa kuna suala linalofanywa na baadhi ya ndugu wenye kupupia juu ya kutendea kazi Sunnah. Watu hawa wanaswali nyuma ya imamu ambaye ana mazowea ya kusoma du´aa ya kumaliza kusoma Qur-aan nzima. Anapofika katika Rak´ah ya mwisho anaondoka na kujitenga na watu kwa hoja kwamba kitendo hicho ni Bid´ah. Hili ni jambo lisilofaa kutokana na ile tofauti na chuki inayopatikana kwa kufanya hivo. Isitoshe hayo ni kinyume na yale wanayoonelea maimamu. Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) alikuwa haonelei kufaa kufanya Qunuut katika swalah ya Fajr. Pamoja na hivyo amesema:

“Mtu anapoongozwa na anayefanya Qunuut katika swalah ya Fajr basi amfuate na pia aitikie “Aamiyn” juu ya du´aa yake.”

Mfano wa hili ni kwamba baadhi ya ndugu wenye upupiaji juu ya kufuata Sunnah kuhusu idadi ya Rak´ah katika swalah ya Tarawiyh wanaposwali nyuma ya imamu anayeswali zaidi ya Rak´ah kumi na moja au Rak´ah kumi na tatu basi wanaondoka ikiwa imamu atazidisha idadi hii. Hiki pia ni kitendo kisichotakikana na pia ni kwenda kinyume na matendo ya Salaf (Radhiya Allaahu ´anhum). Hakika Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) pindi ´Uthmaan bin ´Affaan (Radhiya Allaahu ´anh) aliposwali Minaa kwa kukamilisha hali ya kuwa ni mwenye tafsiri anayotegemea walimkemea kitendo cha yeye kuswali kwa kukamilisha. Hata hivyo walikuwa wakiswali nyuma yake kwa kukamilisha. Miongoni mwa mambo yanayofahamika ni kwamba kuswali kwa kukamilisha katika hali ambayo imesuniwa kufupisha ni ukiukaji mkubwa wa Sunnah kuliko kuzidisha juu ya Rak´ah kumi na tatu. Pamoja na haya yote Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) hawakuwa wakijitenga na ´Uthmaan bin ´Affaan au wakiacha kuswali pamoja naye. Hapana shaka kwamba wao ni wenye pupa ya kufuata Sunnah, maoni bora zaidi kuliko sisi na wenye kushikamana barabara kuliko sisi kwa yale yanayotakiwa na Shari´ah ya Kiislamu.

Tunamuomba Allaah atujaalie sote kuwa miongoni mwa wale wenye kuiona haki na wakaifuata na wakaona batili kuwa ni batili na wakajiepusha nayo.

[1] al-Bukhaariy (6008).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 48 mas-alatu fiy Swiyaam, uk. 35-36
  • Imechapishwa: 27/04/2021