37. Wudhuu´ unachenguka ikiwa umemalizika muda wa kupangusa?

Swali 37: Wudhuu´ unachenguka ikiwa umemalizika muda wa kupangusa?

Jibu: Wudhuu´ hauchenguki kwa kumalizika kwa muda. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliweka muda wa kupangusa na si kumalizika kwa twahara. Kilichowekewa muda sio ile twahara mpaka tuseme kuwa ukimalizika muda wa kupangusa basi twahara inachenguka. Kilichowekewa muda maalum ni ule upangusaji. Ukimalizika muda uliowekwa wa kupangusa usipanguse. Lakini ukifuta kabla ya kumalizika muda wa kupangusa na bado uko na twahara, basi twahara hii bado ni yenye kusihi kwa mujibu wa dalili ya ki-Shari´ah. Kilichokamilika kwa mujibu wa dalili ya ki-Shari´ah hakichenguki isipokuwa kwa mujibu wa dalili ya ki-Shari´ah. Hapa hakuna dalili juu ya hilo. Kimsingi ni kwamba twahara bado ni yenye kubaki na haijachenguka.

Inapokuja katika masuala ya kuchenguka, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwawekea msingi bwana mmoja alipomwambia kuwa anahisi kitu ndani ya swalah yake:

“Asitoke mpaka asikie sauti au ahisi harufu.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwajibisha kutawadha isipokuwa mpaka mtu ayakinishe kweli kuwa umechenguka. Hapana tofauti kati ya kwamba kile kinachotiliwa shaka ni jambo la wajibu au hukumu ya ki-Shari´ah. Katika hali zote mbili inahusiana na ujinga; mtu wa kwanza hajui kama kumetokea kitu au hakukutokea na mtu wa pili hajui kama Shari´ah inawajibisha au haiwajibishi. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaposema:

 “Asitoke mpaka asikie sauti au ahisi harufu.”

basi inapata kutambulika kuwa wudhuu´ wake hauchenguki isipokuwa mpaka kuwepo yakini. Katika hali hii hakuna yakini na hivyo twahara yake bado ni yenye kuendelea.

[1] al-Bukhaariy (137) na Muslim (361).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Buhuuth wa Fataawaa fiyl-Mas´h ´alaal-Khuffayn, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (11/179-180)
  • Imechapishwa: 06/05/2021