36. Ndio maana ´ibaadah ya usiku ikawa bora zaidi

Hakika swalah ya usiku na kisomo chake kimepewa uzito zaidi kwa sababu hukusanya moyo zaidi, huwa mbali na mambo ya kumshughulisha na kumghafilisha, harakati za mahitaji na ni kinga zaidi dhidi ya kujionyesha na mengineyo katika yanayoharibu matendo, pamoja na yale yaliyokuja katika Shari´ah ya kuwepo kwa kheri usiku. Kwani kusafirishwa usiku kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kulikuwa usiku. Isitoshe amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Anateremka Mola wenu kila usiku kwenye mbingu ya dunia wakati unapopita nusu ya usiku  na anasema: ”Je, yupo muombaji Nimuitikie?”[1]

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Katika usiku kuna saa ambayo Allaah huitikia du´aa ndani yake kila usiku.”[2]

Mtunzi wa ”Bahjat-ul-Asraar” amesimulia kutoka kwa Salmaan al-Anmaatiy, ambaye amesema:

”Nilimuona ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) katika ndoto akisema:

Lau si kwa wale wenye nyuradi wanasimama usiku

na wengine wenye mfululizo wanafunga

Ningelibomoa ardhi yenu kutoka chini yenu alfajiri

kwa sababu nyinyi ni watu wabaya hamtii

Tambua ya kwamba fadhilah ya kusimama usiku na kusoma ndani yake hupatikana kwa kidogo na kwa kingi. Kadiri inavyokuwa nyingi ndivyo ilivyo bora zaidi, isipokuwa akeshe usiku wote. Kwani kuendelea kufanya hivyo kunachukizwa au kama itamdhuru nafsi yake. Katika yanayoonyesha kupatikana kwake kwa kidogo ni Hadiyth ya ´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aasw (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kusimama kuswali kwa Aayah kumi hataandikwa miongoni mwa walioghafilika, mwenye kusimama kuswali kwa Aayah mia ataandikwa miongoni mwa wanyenyekevu na mwenye kusimama kuswali kwa Aayah elfu ataandikwa miongoni mwa walioadilifu.”[3]

Ameipokea Abu Daawuud na wengineo.

ath-Tha´labiy ameeleza kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) aliyesema:

”Mwenye kuswali usiku Rak´ah mbili, basi amelala hali ya kuwa amemsujudia Allaah na amesimama kwa ajili Yake.”

[1] al-Bukhaariy (1145) na Muslim (758).

[2] Muslim (757).

[3] Abu Daawuud (1398). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (1398).

  • Muhusika: Imaam Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy (afk. 677)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tibyaan fiy Aadaabi Hamalat-il-Qur-aan, uk. 43-45
  • Imechapishwa: 26/08/2026