35. Mwanaume anapaswa kuvaa nguo iliyo juu ya kongo mbili za miguu

238 – Ibn Abiy Shaybah ametuhadithia: Bakr bin ´Ubayd – Qadhiy wa Kuufah – ametuhadithia, kutoka kwa ´Iysaa bin al-Mukhtaar, kutoka kwa Ibn Abiy Laylaa, kutoka kwa Ibn Buraydah, kutoka kwa baba yake, aliyesimulia kwamba Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mtu atakayeburuta nguo yake kwa majivuno, basi Allaah (´Azza wa Jall) hatamtazama siku ya Qiyaamah.”[1]

239 – Ishaaq bin Ismaa´iyl ametuhadithia: Sufyaan ametuhadithia: Tumemsikia Zayd bin Aslam akisema:

”Niliingia kwa ´Abdullaah bin ´Umar ambapo ´Abdullaah bin Waahid akapita mbele yake akiwa amevaa vazi jipya, nikamsikia akisema: ”Ee mwanangu, pandisha kikoi chako; kwani mimi nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema: Allaah (´Azza wa Jall) hatamtazama mtu anayeburuta kikoi chake kwa majivuno.”

240 – Abu Yaasir ´Ammaar bin Naswr al-Marwaziy ametuhadithia: Baqiyyah bin al-Waliyd ametuhadithia, kutoka kwa Khaalid bin Abiy Bakr, ambaye amesema:

”Alipita kijana mmoja akiwa na vazi zuri juu yake, akamuita na kusema: ”Ee mwana wa Aadam ambaye unajiona kwa sababu ya ujana wako na unajiona kwa sababu ya uzuri wako. Kana kwamba kaburi limekwishafunika mwili wako na kana kwamba umekwishakutana na matendo yako. Ole wako! Tibu moyo wako, kwani haja ya Allaah (´Azza wa Jall) kwa waja ni wao kuzitengeneza nyoyo zao.”

241 – Abul-Hasan ash-Shaybaaniy amenihadithia: Mzee mmoja ametuhadithia:

”´Umar bin ´Abdul-´Aziyz alihiji kabla hajawa khaliyfah. Twaawuus akamuona na yeye huku anatembea kwa majivuno katika mwendo wake, akamfinya ubavuni mwake kwa kidole chake na kusema: ”Hii si mwendo wa mwenye uchafu tumboni mwake.” Ndipo ´Umar akasema hali ya kuomba udhuru: ”Ee ami yangu! Kila kiungo changu kimepigwa ili kiwe katika mwendo huu mpaka nikauzowea.”

242 – Ahmad bin Ibraahiym ametuhadithia: Abu Daawuud amenihadithia: Hammaad bin Salamah ametuhadithia, kutoka kwa Thaabit, ambaye amesema:

”Swilah bin Ashyam na wenzake walimuona mtu amevaa kikoi chake chini ya kongo mbili za miguu, ambapo wakataka wenzake wamkemee kwa ndimi zao. Ndipo Swilah akasema: ”Niacheni nikutoshelezeni.” Akamwambia: ”Ee mtoto wa ndugu yangu, hakika mimi nina haja nawe.” Akasema: ”Nini hiyo, ee ami?” Akasema: ”Pandisha kikoi chako.” Akasema: ”Ndio, tena kwa furaha.” Akawaambia wenzake: ”Hivo ni bora kuliko kumwendea moja kwa moja na akaleta ushindani.”

243 – Mufadhdhwal bin Ghassaan amenihadithia, kutoka kwa baba yake, ambaye amesema:

”Mfanya ´ibaadah al-´Umariy alimwona mtu katika familia ya ´Aliy anatembea kwa majivuno, akamwendea kwa haraka, akamshika kwa mkono wake na kumwambia: ”Ee huyu, hakika yule ambaye Allaah (´Azza wa Jall) amekukirimu kwa utukufu wake hakuwa na mwendo huu.” Basi yule mtu akaacha baada ya hapo.”

244 – ´Abdullaah bin ´Iysaa at-Twafaawiy ametuhadithia: Muhammad bin ´Abdillaah az-Zarraad ametuhadithia:

”Muhammad bin Waasiy´ alimwona mwanawe akijipiga mikono yake kwa majivuno, akamuita akamwambia: ”Je, unajua wewe ni nani? Ama kuhusu mama yako nilimnunua kwa dirhamu 200. Kuhusu baba yako namwomba Allaah (´Azza wa Jall) asiumbe waislamu wengi mfano wake.”

[1] al-Bukhaariy (3665) na Muslim (2085).

  • Muhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa (afk. 281)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Khumuul wat-Tawaadhwu´, uk. 284-289
  • Imechapishwa: 30/03/2026