Katika zama hizi zilizoharibika ima mtu akajichagulia mwenyewe kuwa ni mwanachuoni mbele ya Allaah au akawa ni mwanachuoni kwa watu wa zama zake. Ikiwa atachagua hilo la kwanza basi atosheke na utambuzi wa Allaah juu yake. Yule mwenye utambuzi kati yake yeye na Allaah basi hutosheka na utambuzi wa Allaah juu yake. Na yule asiyeridhia isipokuwa azingatiwe kuwa ni mwanachuoni mbele za watu basi ataingia ndani ya maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule mwenye kujifunza elimu kwa ajili ya kujifakharisha kwa wanazuoni, kugombana na wapumbavu au kutaka kuyageuza macho ya watu wamwangalie yeye, basi ajiandalie makazi yake Motoni.”[1]

Wuhayb bin Ward amesema:

“Huenda mtu akazingatiwa na watu kuwa mwanachuoni ilihali Allaah akamjumuisha ni katika wajinga.”[2]

Muslim amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah aliyesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wa mwanzo watakaotupwa Motoni ni watu aina tatu. Mmoja wao, ni mtu ambaye amejifunza elimu na akaifunza na akasoma Qur-aan. Ataletwa na kujuzwa neema yake. Aseme: “Nimezitambua.” Aulizwe: “Ulifanya nini kwayo?” Aseme: “Nilijifunza elimu na mimi nikaifunza na nikasoma Qur-aan kwa ajili Yako.” Ataambiwa: “Umesema uongo. Hakika wewe ulijifunza ili uitwe ‘mwanachuoni’ na umesoma Qur-aan ili isemwe ‘msomaji’ na kumeshasemwa. Baada ya hapo kuamrishwe atupwe kwa uso wake ndani ya Moto.”[3]

[1]at-Tirmidhiy (2655). Swahiyh kupitia nyenginezo kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (106).

[2]Hilyat-ul-Awliyaa’ (8/157).

[3]Muslim (1905).

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 88-90
  • Imechapishwa: 30/09/2021