35. Kuswali nyuma ya anayetafuta baraka kwenye makaburi

Swali: Ni ipi hukumu ya kuswali nyuma ya anayeenda kwenye makaburi ya waja wema kwa ajili ya kutafuta baraka kwayo na kusoma Qur-aan katika mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwenginepo kwa kupokea malipo juu ya hilo?

Jibu: Haya yanahitaji upambanuzi. Ikiwa ni kwa kusherehekea peke yake pasi na shirki basi huyu ni mzushi. Haitakikani akawa imamu kutokana na yale yaliyothibiti katika Hadiyth Swahiyh kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Nakutahadharisheni na mambo yaliyozuliwa. Kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotofu.”[1]

Kusherehekea mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Bid´ah.

Lakini ikiwa anawaomba wafu na anawataka uokozi au majini au viumbe wengine na anasema ´ee Mtume wa Allaah! Ninusuru! Mponye mgonjwa wangu!` au anasema ´ee bwana al-Husayn! Ee bwana al-Badawiy!` au wafu wengine au viumbe visivyokuwa na uhai kama vile masanamu ´niokoeni`, basi huyu ni mshirikina shirki kubwa. Haifai kuswali nyuma yake na wala hausihi uimamu wake. Tunamuomba Allaah afya.

Lakini ikiwa wanafanya Bid´ah, kama vile kuhudhuria mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) lakini hafanyi shirki, anasoma Qur-aan au kuswali makaburini na hafanyi shirki, basi huyu amefanya uzushi katika dini. Afundishwe na aelekezwe katika kheri na swalah yake ni sahihi muda wa kuwa haikuiswali kwenye makaburi. Kuhusu kuswali makaburini swalah haisihi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Allaah awalaani mayahudi na manaswara. Wameyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni mahali pa kuswalia.”

Kuna maafikiano juu yake[2].

[1] Ahmad (16694), Abu Daawuud (4607) na Ibn Maajah (46).

[2] al-Bukhaariy (436) na Muslim (529).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 122-123
  • Imechapishwa: 19/07/2022