162 – Tambua kuwa Allaah (Ta´ala) hana anayelingana Naye kwa njia yoyote ile. Yule mwenye kumfananisha Allaah na viumbe Wake, basi amekufuru na kula khasara. Lakini hiyo haina maana ya kukanushwa sifa Zake zilizotakasika. Yeye ndiye Mungu Mtukufu anayesifika kwa sifa Alizojieleza Mwenyewe kupitia Mitume Yake (´alayhimus-Salaam). Allaah (Ta´ala) alisema kumwambia Muusa na ndugu yake:

قَالَ لَا تَخَافَا ۖ إِنَّنِي مَعَكُمَا أَسْمَعُ وَأَرَىٰ

“Hakika Mimi Niko pamoja nanyi, Nasikia na Naona.”[1]

Allaah (Ta´ala) ameeleza kwamba Ibraahiym (´alayhis-Salaam) amesema:

يَا أَبَتِ لِمَ تَعْبُدُ مَا لَا يَسْمَعُ وَلَا يُبْصِرُ وَلَا يُغْنِي عَنكَ شَيْئًا

“Ee baba yangu! Kwa nini unaabudu vile visivyosikia na visivyoona na visivyokufaa kitu chochote?”[2]

Allaah (Ta´ala) amesema:

مَّن كَانَ يُرِيدُ ثَوَابَ الدُّنْيَا فَعِندَ اللَّـهِ ثَوَابُ الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ سَمِيعًا بَصِيرًا

”Anayetaka thawabu za dunia, basi kwa Allaah kuna thawabu za dunia na Aakhirah. Na Allaah daima ni Mwenye kusikia, Mwenye Kuona.”[3]

وَكَانَ اللَّـهُ سَمِيعًا عَلِيمًا

”Na Allaah daima ni Mwenye kusikia, Mjuzi wa kila jambo.”[4]

وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا

”Na Allaah daima ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu. ”[5]

Kuna Aayah nyingi mfano wa hizo zinazothibitisha usikizi wa milele, uoni na msamaha ambazo zinasambaratisha wale wanaomfananisha, kwa sababu alikuwa na sifa zote hizi kabla ya kupatikana vinavyosikia, vinavyoona na vinavyosamehewa. Yuko hivi sasa kama ambavyo daima Alikuwa na Yeye ndiye Mfalme wa siku ya Malipo. Yeye (Ta´ala) daima na milele ni Mwenye kusifiwa kwa sifa hizi. Anazo sifa kuu na majina mazuri mno kikweli na si kwa njia ya mafumbo (مجازا). Kwa ajili hiyo Alikuwa Muumbaji na Mruzukaji kabla ya kuumba na kuruzuku chochote. Kisha baada ya kupwekeka na umoja Wake, Akaumba viumbe avitakavyo. Akachagua na kutaka kuwepo kwa viumbe wanaompwekesha na kumsabihi. Allaah (Ta´ala) amesema:

تُسَبِّحُ لَهُ السَّمَاوَاتُ السَّبْعُ وَالْأَرْضُ وَمَن فِيهِنَّ ۚ وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلَّا يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ وَلَـٰكِن لَّا تَفْقَهُونَ تَسْبِيحَهُمْ ۗ إِنَّهُ كَانَ حَلِيمًا غَفُورًا

“Zinamsabihi mbingu saba na ardhi na vilivyomo ndani yake; hakuna kitu chochote isipokuwa kinamtukuza kwa himdi Zake, lakini hamzielewi tasbihi zao. Hakika Yeye ni mvumilivu, Mwingi wa kusamehe.”[6]

Viumbe wote wanampwekesha na kumtukuza Muumbaji Wake na kunyenyekea amri Yake:

تُسَبِّحُ لَهُ السَّمَاوَاتُ السَّبْعُ وَالْأَرْضُ وَمَن فِيهِنَّ ۚ وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلَّا يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ وَلَـٰكِن لَّا تَفْقَهُونَ تَسْبِيحَهُمْ

“Zinamsabihi mbingu saba na ardhi na vilivyomo ndani yake na hakuna kitu chochote isipokuwa kinamtukuza kwa himdi Zake, lakini hamzifahamu Tasbiyh zao.”[7]

[1] 20:46

[2] 19:42

[3] 4:134

[4] 4:148

[5] 4:96

[6] 17:44

[7] 17:44

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy (afk. 748)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Arba´iyn fiy Swifaati Rabb-il-´Aalamiyn, uk. 165-166
  • Imechapishwa: 11/06/2024