34. Mavazi ya majivuno na mwendo wa maringo

232 – Muhammad bin Bakkaar ametuhadithia: ´Abdur-Rahmaan bin Abiyz-Zinaad ametuhadithia, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa al-A´raj, kutoka kwa Abu Hurayrah, ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Allaah hatamtazama siku ya Qiyaamah mtu anayevuta kikoi chake kwa kiburi.”[1]

233 – Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tena:

”Wakati mtu mmoja alikuwa akitembea kwa maringo akiwa amevaa nguo mbili hali kujiona nafsi yake, Allaah akafanya ardhi kummeza. Basi ataendelea kuzama humo mpaka siku ya Qiyaamah.”[2]

234 – Ibn Jamiyl ametuhadithia: ´Abdullaah ametukhabarisha: Yuunus ametukhabarisha, kutoka kwa az-Zuhriy: Saalim ametukhabarisha, kutoka kwa Ibn ´Umar, ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Wakati mtu mmoja alikuwa akijitingisha katika mwendo wake, Allaah akafanya ardhi kummeza. Basi ataendelea kuzama humo mpaka siku ya Qiyaamah.”

235 – ´Ammaar bin Naswr ametuhadithia: Baqiyyah bin al-Waliyd ametuhadithia, kutoka kwa al-Haytham bin Maalik at-Twaa-iy, kutoka kwa ´Abdur-Rahmaan bin ´Aa-idh, kutoka kwa Abul-Hajjaaj ath-Thamaaliy, aliyeeleza kwamba Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Kaburi humwambia maiti anapowekwa ndani yake: ”Ole wako ee mwanaadamu, nini kilikudanganya juu yangu? Je, hukuwa unajua kuwa mimi ni nyumba ya mtihani, nyumba ya giza, nyumba ya upweke na nyumba ya minyoo? Nini kilikudanganya juu yangu? Ulikuwa unapita mbele yangu kwa kupepeta mguu wako.”

Ibn ´Aai-dh akasema: ”Ee Abu al-Hajjaaj, pepeto ni nini?” Akasema: ”Ni anayekanyaga mguu mmoja mbele na mwingine nyuma, kama mwendo wa mpwa wako mara nyingine.” Kipindi hicho alikuwa anavaa na kujipamba.”

236 – Ibn Jamiyl ametuhadithia: ´Abdullaah ametukhabarisha: Ma´mar ametukhabarisha: Yahyaa bin al-Mukhtaar amenihadithia, kutoka kwa al-Hasan, ambaye amesema:

”Unamkuta mmoja wao akijitingisha katika mwendo wake, akivuta mifupa yake mfupa baada ya mfupa. Hatembei kawaida yake.”

 237 – Ahmad bin Ibraahiym bin Kathiyr ametuhadithia: Hajjaaj bin Muhammad ametuhadithia, kutoka kwa Abu Bakr al-Hudhaliy, ambaye amesema:

”Tulipokuwa pamoja na al-Hasan basi Ibn-ul-Ahtamm alipita. Alikuwa njia akielekea Maqsuurah, alikuwa amevaa makoti ya hariri yaliyowekwa mengine juu ya mengine miguuni mwake, na shati lake likawa limefunguka, naye akitembea kwa maringo. al-Hasan akamtazama kisha akasema: ”Ole wako! Unajivuna kwa pua yako – unageuza shingo yako, unapinda shavu lako, unatazama pande zako mbili, ee mpumbavu ulioje! Unatazama pande zako katika neema ambazo hazishukuriwi wala kukumbukwa? Hukuwa miongoni mwa waliotekeleza amri ya Allaah (´Azza wa Jall) humo, wala waliotoa haki ya Allaah humo. Naapa kwa Allaah! Hapana mtu anayejitembeza kwa asili yake isipokuwa hujitingisha kama mwendawazimu. Katika kila kiungo chake kuna neema ya Allaah na kwa shaytwaan kuna laana.” Ibn-ul-Ahtamm aliposikia akarudi kuomba msamaha, akasema: ”Usiniombe msamaha, bali tubia kwa Mola wako (´Azza wa Jall). Je, hujasikia maneno ya Allaah (´Azza wa Jall) aliposema:

وَلَا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا ۖ إِنَّكَ لَن تَخْرِقَ الْأَرْضَ وَلَن تَبْلُغَ الْجِبَالَ طُولًا

”Wala usitembee katika ardhi kwa majivuno; hakika wewe huwezi kuipasua ardhi na wala huwezi kufikia urefu wa milima.”?[3]

[1] al-Bukhaariy (5788) na Muslim (2087).

[2] al-Bukhaariy (3485) na Muslim (2088).

[3] 17:37

  • Muhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa (afk. 281)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Khumuul wat-Tawaadhwu´, uk. 276-283
  • Imechapishwa: 30/03/2026