34. Maana ya kulingana juu inatambulika na namna yake haitambuliki

Kwa hiyo kulingana kunajulikana na kwamba maana yake ni kuwa juu na kuinuka juu. Namna haijulikani na hakuna anayejua namna zilivyo sifa Zake isipokuwa Yeye Mwenyewe (Subhaanahu wa Ta´ala). Amelingana juu ya ´Arshi bila ya namna. Hushuka kwenye mbingu ya chini bila ya namna. Huridhia na hughadhibika bila ya namna. Huchukia bila ya namna. Atakuja siku ya Qiyaamah bila ya namna. Hivi ndivyo wanavyoamini Ahl-us-Sunnah. Hakuna anayejua namna zilivyo sifa Zake isipokuwa Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala). Ni sifa za haki na zilizothibiti. Ni wajibu kumthibitishia nazo Allaah kwa njia inayolingana Naye. Hafananishwi na viumbe Vyake kwenye kitu katika sifa Zake (Jalla wa ´Alaa). Amesema (Subhaanah):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”

فَلَا تَضْرِبُوا لِلَّـهِ الْأَمْثَالَ ۚ

”Basi msipigie mifano Allaah!” (16:74)

Ni kama kusema kwamba anafanana na kitu kadhaa. Amesema (Ta´ala):

هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا

“Je, unamjua [mwengine] mwenye jina kama Lake?” (19:65)

Bi maana hakuna anayelingana Naye, kushabihiana Naye na wala hana mwenza (Subhaanahu waTa´ala). Haya ndio maoni ya Ahl-ul-Haqq; ambapo wanaamini kuwa yuko juu, yuko juu ya ´Arshi, amelingana juu yake kulingana ambako kunalingana na utukufu Wake na ukubwa Wake. Yeye hafananishwi na viumbe Vyake katika kulingana kwao, kushuka kwao, kucheka kwao, kukasirika kwao na sifa nyenginezo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 48
  • Imechapishwa: 22/10/2024