34. Kitenguzi cha pili: Kuweka mkatikati baina yako na Allaah

Shaykh na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

La pili:

Atakayeweka baina yake yeye na Allaah wakatikati ambapo anawaomba na anawaomba wamshufaie na akawategemea, amekufuru kwa maafikiano.

MAELEZO

Mwandishi (Rahimahu Allaah) amesema:

“La pili” – Bi maana miongoni mwa vitenguzi vya Uislamu. Akaendelea kusema:

“Atakayeweka baina yake yeye na Allaah wakatikati ambapo anawaomba na anawaomba wamshufaie na akawategemea, amekufuru kwa maafikiano.”

Wakatikati – Bi maana katika viumbe ambao wanawakalia kati baina yao na Allaah kwa madai yao. Haya masuala ya ukatikati baina ya Allaah na viumbe Wake yanahitajia ufafanuzi[1], kama alivyosema Shaykh-ul-Islaam[2]:

“Mwenye kusema kwamba lazima tuwe na mkatikati baina ya Allaah na viumbe Wake. Ataulizwa kwanza: “Nini makusudio yako na mkatikati?” Ikiwa makusudio yake ni kwamba lazima kuwepo na mkatikati katika kufikisha Ujumbe baina yetu na baina ya Allaah, hili ni kweli. Ukatikati huu ni wa lazima na mwenye kuupinga anakufuru. Lazima kuwepo na mkatikati baina ya Allaah na viumbe Vyake katika kufikisha Shari´ah Yake. Nao si wengine ni Mitume (´alayhimus-Swalaah wa sallam). Wao ndio wakati na kati baina yetu sisi na Allaah. Wakusudiwa ni Mitume katika jinsia ya Malaika na watu. Wao ndio wakatikati baina yetu sisi na Allaah. Mwenye kupinga ukatikati huu anakufuru. Kwa msemo mwingine mwenye kuwapinga Malaika na Mitume ambao wanatuletea Shari´ah ya Allaah na akasema hatuna haja yao na kwamba sisi tunawasiliana na Allaah pasi nao – kama wanavyosema Suufiyyah waliopindukia – kwamba wao wanapokea (Shari´ah) moja kwa moja kutoka kwa Allaah bila ya wakatikati, hii ni kufuru kwa maafikiano.

Kuna ukatikati ambao yule mwenye kuuthibitisha anakufuru, nao ndio ni ule aliousema Shaykh (Rahimahu Allaah). Nao ni mtu kujiwekea ukatikati baina ya Allaah na viumbe Wake ambapo akawa anawaomba, anawaomba uombezi, anawategemea, ukatikati huu yule mwenye kuuthibitisha anakufuru kwa maafikiano. Kwa sababu hakuna ukatikati baina yetu sisi na Allaah inapokuja katika kumuabudu. Bali ni wajibu kwa mtu kumuabudu Allaah moja kwa moja, tumuombe moja kwa moja pasi na mkatikati, tumuombe uombezi moja kwa moja pasi na mkatikati, tumtegemee Yeye pasi na mkatikati. Mambo yanatakiwa kuwa baina yetu sisi na Allaah.  Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ

“Mola wenu amesema: “Niombeni Nitakuitikieni.” (Ghaafir 40:60)

Hakusema “Niombeni kwa kupitia kwa fulani” au kwamba “Fanyeni mkatikati”. Ukatikati huu yule mwenye kuuthibitisha amekufuru. Nao ni kuweka baina yake yeye na Allaah wakatikati ambapo akawa anawatekelezea kitu katika ´ibaadah ili wamkurubishe kwa Allaah, kama walivyokuwa wanasema washirikina hapo kabla:

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

”Wanaabudu badala ya Allaah ambao hawawezi kuwadhuru na wala kuwanufaisha na huku wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.” (Yuunus 10:18)

Ameita kitendo hichi kuwa ni ´ibaadah:

قُلْ أَتُنَبِّئُونَ اللَّـهَ بِمَا لَا يَعْلَمُ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ

“Je, mnamjulisha Allaah kwa yale asiyoyajua katika mbingu na ardhini?  Kutakasika kutokamana na mapungufu na kutukuka ni Kwake kutokamana na yale yote wanayomshirikisha.” (Yuunus 10:18)

Ameita kitendo hiki kuwa ni shirki na ameitakasa nafsi Yake nacho. Hii ndio hali ya waabudu wa wafu na waabudu wa makaburi hii leo. Wanawafanya mawalii na watu wema kuwa wakatikati baina yao na baina ya Allaah ambapo wanawachinjia kwenye makaburi yao, wanawawekea nadhiri, wanawataka uokozi na wanawaomba badala ya Allaah. Wakiambiwa hii ni shirki wanasema wanapinga na kusema kwamba hawa ni waombezi wetu tu baina yetu na Allaah. Wanasema kwamba wao hawaitakidi kuwa wao wanaumba pamoja na Allaah, wanaruzuku pamoja na Allaah au wanaendesha mambo pamoja na Allaah, isipokuwa tunawafanya tu kuwa ni wakati na kati baina yetu na baina Allaah, wanamfikishia Allaah haja zetu. Matokeo yake wanawachinjia, wanawaadhimisha, wanawawekea nadhiri kwa hoja kuwa ni wakati na kati baina yao na baina ya Allaah. Hii ndio shirki ya wale watu wa kale. Amesema (Ta´ala):

وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ إِنَّ اللَّـهَ يَحْكُمُ بَيْنَهُمْ فِي مَا هُمْ فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي مَنْ هُوَ كَاذِبٌ كَفَّارٌ

”Wale waliojichukulia badala Yake walinzi [na huku wakisema]: “Hatuwaabudu isipokuwa kwa lengo la kutukurubisha kwa Allaah ukaribu.” Hakika Allaah atahukumu baina yao katika yale yote waliyokhitilafiana nayo. Hakika Allaah hamwongoi aliye muongo, kafiri.” (az-Zumar 39:03)

Ama yule mwenye kuweka wakatikati na akaitakidi kuwa wao ni sababu tu na wala hawaombi, hawachinjii wala hawawekei nadhiri. Bali tu anaitakidi kuwa ´ibaadah ni ya Allaah na wala hamuabudu mwingine isipokuwa Allaah pekee, lakini akajiwekea mkatikati kwa kuwa ni sababu miongoni mwa sababu kwa madai yake, hii ni Bid´ah na njia inayopelekea katika shirki. Kwa kuwa Allaah hakutuamrisha kuweka wakatikati katika kuomba du´aa au kuomba uombezi na wala hii sio sababu na wala Allaah hakufanya ikawa ni sababu ya kupokelewa kwa du´aa eti umejiwekea mkatikati baina yako wewe na Allaah ambaye ni mja mwema miongoni mwa waja wema, Mtume au wengineo. Huku ni kumsemea Allaah pasi na elimu. Allaah ameamrisha kumuomba na wala hakutuamrisha kuweka wakatikati baina yetu sisi na Yeye.

[1] Tazama ”Majmuu´-ul-Fataawa” (01/121-123).

[2] Tazama ”Majmuu´-ul-Fataawa” (01/121-123).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 59-61
  • Imechapishwa: 06/08/2018