Tambueni kwamba swawm ina adabu zinazopaswa kuzingatiwa na kujipamba nazo ili swawm iwe inaendana na namna ilivyowekwa katika Shari´ah na ndipo faida zake zipatikane na lengo lake lifikiwe na wala isiwe taabu kwa mwenye kufunga bila faida. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Huenda mfungaji asiwe na kitu katika swawm yake isipokuwa njaa.”[1]

Kwa hiyo swawm si kuacha chakula na kinywaji tu, bali pamoja na hilo ni kuacha maneno na matendo yasiyofaa katika yaliyo haramu au yanayochukiza.

Baadhi ya Salaf wamesema:

”Swawm rahisi zaidi ni kuacha chakula na kinywaji.”

Hakika kujikurubisha kwa Allaah kwa kuacha matamanio yaliyo halali hakutimii isipokuwa baada ya kujikurubisha Kwake kwa kuacha yale Aliyoyaharamisha katika kila hali. Muislamu, japokuwa ni wajibu kwake kuacha haramu katika kila wakati, lakini katika wakati wa funga jambo hilo linakuwa na mkazo zaidi. Yule anayefanya haramu nje ya wakati wa swawm anatenda dhambi na anastahiki adhabu. Akifanya hivyo katika wakati wa swawm, basi pamoja na dhambi na kustahiki adhabu, hilo linaathiri funga yake kwa kupungua au hata kubatilika. Mfungaji wa kweli ni yule aliyefunga tumbo lake dhidi ya chakula na kinywaji, viungo vyake vikafunga dhidi ya madhambi, ulimi wake ukafunga dhidi ya ufidhuli na maneno machafu, masikio yake yakafunga dhidi ya kusikiliza nyimbo, ala za muziki, filimbi, maneno ya mwenye kusengenya na mwenye kueneza umbea na macho yake yakafunga dhidi ya kutazama yaliyo haramu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yule asiyeyaacha maneno ya uongo na kuufanyia kazi, basi Allaah hana haja ya yeye kuacha chakula chake na kinywaji chake.”[2]

Ni wajibu kwa mwenye kufunga ajiepushe na kusengenya, umbea na kutukana. Hilo ni kutokana na yale aliyopokea al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Ikiwa ni siku ya swawm ya mmoja wenu, basi asiseme maneno machafu wala asitende ujinga. Ikiwa mtu atapigana naye au atamtukana, basi aseme: ”Mimi ni mwenye kufunga.”[3]

[1] Ibn Maajah (1690), an-Nasaa´iy (3249), Ahmad (02/373), al-Haakim (01/431), al-Bayhaqiy (04/27). al-Haakim amesema:

”Swahiyh juu ya masharti ya al-Bukhaariy na hawakuipokea.”

na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[2] al-Bukhaariy (1903).

[3] al-Bukhaariy (1894) na Muslim (1151).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tawjiyhaat wa Tanbiyhaat lil-Fataati al-Muslimah, uk. 34
  • Imechapishwa: 28/02/2026