Pindi mtu elimu yake inakuwa si yenye kunufaisha pale anapojiona ni mwenye fadhilah juu ya wale waliotangulia katika maoni au ufaswaha, basi huanza kuona kuwa ni mjuzi zaidi au mwenye ngazi ya juu mbele ya Allaah juu ya wengine. Kwa vile anajiona ana kitu ambacho wengine hawana, basi huanza kuwadharau wale waliomtangulia na kuwatweza kutokana na uchache wa elimu. Masikini huyu hajui kuwa uchache wa maneno ya waliotangulia ilikuwa ni kutokana na kujichunga na kumcha Allaah. Vinginevyo wangelitaka kuzungumza na kurefusha maneno basi wasingeshindwa kufanya hivo. Kama alivosema Ibn ´Abbaas baada ya kuwasikia watu wanaogombana juu ya mambo ya dini:

“Hamjui kuwa Allaah ana waja ambao wamenyamaza kwa ajili ya kumuogopa Allaah? Si wenye kukosa ufaswaha wala sio mabubu. Ni wanazuoni, wafaswaha, wenye kuzungumza vizuri, watukufu. Ni wasomi juu ya matukio ya Allaah, lakini wanapokumbuka utukufu wa Allaah basi hustaajabu, wananyenyekea na kunyamaza. Wanaporudi katika hali yao ya kawaida basi hufanya haraka kwenda kwa Allaah kwa kufanya matendo matukufu. Wanaziona nafsi zao kuwa wazembeaji na wapungufu. Licha ya kwamba ni wenye busara na wenye nguvu dhidi ya watu madhalimu na wakosefu. Ni wema na wasiokuwa na hatia. Hawajikwezi kwa matendo yao mengi kumfanyia Yeye, hawaridhiki kwa yale machache wayanyomfanyia na hawayachukulii matendo yao kuwa ni zawadi Kwake. Pale unapokutana nao basi utawaona kuwa ni wenye wasiwasi, waoga na wenye khofu.”

Ameipokea Abu Nu´aym na wengineo.

Imaam Ahmad na at-Tirmidhiy wamepokea kupitia kwa Abu Umaamah ambaye amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Haya na ukimya ni ngazi mbili za imani, ilihali maneno machafu na ubainifu ni ngazi mbili za unafiki.”[1]

Ni nzuri kwa mujibu wa at-Tirmidhiy na Swahiyh kwa mujibu wa al-Haakim.

Ibn Hibbaan amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Hurayrah kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ubainifu ni wenye kutokana na Allaah na ukimya ni wenye kutokana na shaytwaan. Ubainifu si wingi wa maneno, lakini ubainifu ni kule kupambanua haki. Ukimya si uchache wa maneno, lakini ni kupuuzilia haki.”[2]

Katika cheni ya wapokezi inayokosa Swahabah ameeleza Muhammad bin Ka´b al-Quradhwiy kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Sifa tatu zinamfanya mja kupungukiwa duniani na hivyo kwayo akazidishiwa mengi zaidi huko Aakhirah: udugu, haya na ukimya.”

´Awn bin ´Abdillaah amesema:

“Mambo matatu ni katika imani: haya, kujichunga na machafu na ukimya, na si ukimya wa moyo wala ukimya wa matendo. Mambo haya matatu yanazidisha Aakhirah na yanapunguza duniani. Yale yanayozidisha huko Aakhirah ni makubwa zaidi kuliko yale yanayopunguza duniani.”

Yamepokelewa mfano wa haya kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) lakini kwa njia ambayo ni nyonge.

[1]Ahmad (5/269), at-Tirmidhiy (2027) na al-Haakim (1/9).

[2]Ibn Hibbaan (2010).

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 84-87
  • Imechapishwa: 30/09/2021