33. Tofauti kati ya kumuomba msaada aliye hai mbele yako na asiyekuwa huyo II

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Wana shubuha nyingine. Nayo ni kisa cha Ibraahiym alipotumbukizwa kwenye moto, Jibriyl akamfunulia na kusema: “Je, una haja ya kitu?” Akasema Ibraahiym: “Ama kama ni kutoka kwako, hapana.” Wanasema: “Lau kama kuombwa msaada Jibriyl ni shirki, basi asingejionesha kwa Ibraahiym.” Jibu ni: “Kwa hakika hii ni kama ile shubuha ya kwanza. Kwa hakika Jibriyl alijionyesha kwake ili kumnufaisha kwa kitu ambacho anakiweza, kwani hakika yeye ni kama Allaah alivyomzungumza:

شَدِيدُ الْقُوَىٰ

”Mwenye nguvu kwelikweli.” (an-Najm 53 : 05)

Lau Allaah angelimruhusu kuchukua moto wa Ibraahiym, ardhi na milima na kuvitupa mashariki au magharibi, angelifanya hivyo. Na lau Alingelimuamrisha kumuweka Ibraahiym (´alayhis-Salaam) mahali ambapo ni mbali na wao, angelifanya hivyo. Na lau Angelimuamrisha kumpandisha mbinguni, angalifanya. Hili ni kama mfano wa mtu tajiri ana mali nyingi na ameona mtu mwenye kuhitajia. Akajitolea kumpa mkopo au kumpa kitu atatue kwazo haja yake. Lakini yule mwenye kuhitajia akakataa kuzichukua na akasubiria Allaah kumpa riziki yake mwenyewe. Hili lina mafungamano yepi na kuomba msaada wa ki-´Ibaadah na shirki, lau wangelikuwa wanafahamu?

Tunakhitimisha maneno, Allaah (Ta´ala) akitaka, kwa masuala makubwa ambayo ni muhimu sana yanayofahamika kupitia yale tuliyotangulia tuliyotaja, lakini tutayagawa kutokana na ukubwa wake na kutokana na makosa yanayofanywa ndani yake.

Tunasema: “Hakuna tofauti ya kwamba Tawhiyd lazima iwe kwa moyo, ulimi na ´amali. Mtu akiacha kitu katika haya, hawi Muislamu. Akiijua Tawhiyd na asiifanyie kazi, ni kafiri mwenye inadi, kama kufuru ya Fir´awn na Iblisi na mfano wao. Hili hukosea watu wengi. Wanasema: “Kwa hakika hii ni haki. Tunafahamu hili na tunashuhudia ya kwamba ni haki, lakini hatuwezi kulifanya na watu wa mji wetu hayajuzu isipokuwa yale yenye kuafikiana na wao tu”, au mfano wa nyudhuru kama hizo. Na wala masikini huyu hajui kuwa wengi wa viongozi wa kufuru wanaijua haki na wanaiacha kwa kitu katika nyudhuru. Kama alivyosema (Ta´ala):

اشْتَرَوْا بِآيَاتِ اللَّـهِ ثَمَنًا قَلِيلًا

”Wamenunua Aayah za Allaah kwa thamani ndogo.” (at-Tawbah 09 : 09)

Na mfano wa Aayah kama hizo. Kama Kauli Yake:

يَعْرِفُونَهُ كَمَا يَعْرِفُونَ أَبْنَاءَهُمْ

”Wanamtambua kama wanavyowatambua watoto wao.” (al-Baqarah 02 : 146)

Akiifanyia kazi Tawhiyd kwa matendo ya dhahiri bila ya kuifahamu na wala haiamini ndani ya moyo wake, ni mnafiki na ni mtu wa shari kuliko kafiri wa kweli.

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ فِي الدَّرْكِ الْأَسْفَلِ مِنَ النَّارِ

“Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka la chini kabisa Motoni.” (an-Nisaa´ 04 : 145)

Na haya ni masuala ambayo ni makubwa na marefu yanakubainikia ukiyafikiria kwenye maneno ya watu. Utaona mtu mwenye kujua haki na anaacha kuifanyia kazi, kwa kukhofia maisha ya dunia au nafasi au anataka kumpaka mtu mafuta. Hali kadhalika utaona wenye kuifanyia kazi kwa nje na si kwa undani. Ukiwauliza nini wanachoitakidi ndani ya moyo, hawajui.

Lakini ni juu yako kufahamu Aayah mbili katika Kitabu cha Allaah: ya kwanza ni Kauli Yake (Ta´ala):

لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Msitoe udhuru! Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.” (at-Tawbah 09 : 66)

Ukielewa ya kwamba baadhi ya Maswahabah ambao walipigana vita warumi wakiwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikufuru kwa sababu ya maneno ambayo waliyatamka kwa njia ya utani na mzaha, hapo ndipo itakubainikia ya kwamba yule mwenye kutamka kwa neno la kufuru na akalifanyia kazi kwa kuchelea mali yake isipungue au cheo au kwa sababu anataka kumpaka mtu mafuta, ni jambo baya zaidi kuliko yule ambaye [kakufuru kwa] kuongea kwa maneno ambayo anafanya nayo mzaha. Aayah ya pili ni Kauli Yake (Ta´ala):

مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللَّـهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اسْتَحَبُّوا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا عَلَى الْآخِرَةِ

“Atakayemkufuru Allaah baada ya kuamini kwake [yuko hatiani] – isipokuwa yule aliyelazimishwa na huku moyo wake umetua juu ya imani, lakini aliyekifungulia ukafiri kifua chake – basi hao wana ghadhabu kutoka kwa Allaah na watapata adhabu kubwa. Hivyo ni kwa sababu wao wamefadhilisha maisha ya dunia kuliko ya Aakhirah.” (an-Nahl 16 : 106-107)

Allaah Hakuwapa udhuru watu hawa, isipokuwa yule aliyelazimishwa na huku moyo wake umetua juu ya imani. Kuhusu mwengine asiyekuwa huyu, amekufuru baada ya kuamini kwake, sawa ikiwa kafanya hilo kwa ajili ya khofu, tamaa ya kimaisha, kutaka kumpaka mtu mafuta, cheo kwa watu wa nchi yake, jamaa zake au kwa ajili ya mali yake, au kafanya hilo kwa mzaha au sababu zingine miongoni mwa sababu – isipokuwa tu yule aliyelazimishwa. Aayah inafahamisha hivi kwa mitazamo miwili: ya kwanza ni Kauli Yake:

إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ

“… isipokuwa yule aliyelazimishwa… “

Allaah (Ta´ala) hakumvua yeyote isipokuwa tu yule aliyelazimishwa, na ni jambo linalojulikana ya kwamba mtu hatenzwi nguvu isipokuwa katika maneno au kitendo. Ama itikadi iliyoko moyoni, hakuna anayetenzwa nguvu kwa hilo. Ya pili ni Kauli Yake (Ta´ala):

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اسْتَحَبُّوا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا عَلَى الْآخِرَةِ

“… hivyo ni kwa sababu wao wamefadhilisha maisha ya dunia kuliko ya Aakhirah.”

Kwa hiyo ameweka wazi ya kwamba kukufuru huku na adhabu sio kwa sababu ya kuitakidi, ujinga, kuichukia dini au kupenda kufuru, isipokuwa sababu yake ni kwa ajili ya kutaka kupata sehemu katika mambo ya dunia na kwa ajili hiyo akayapa kipaumbele juu ya dini.

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ndiye Anajua zaidi. Himdi zote anastahiki Allaah, Moal wa walimwengu. Swalah na Salaam zimwendee Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wake wote.

MAELEZO

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) anasema kwamba washirikina wana shubuha nyingine mbali na zile zilizotangulia ambazo tayari zimejibiwa. Nayo ni kwamba Ibraahiym wakati alipotupwa ndani ya moto historia inasema kwamba Jibriyl alijionyesha kwake na akamuuliza kama yuko na haja ambapo akamwambia kwamba hataki msaada kutoka kwake lakini hata hivyo yuko tayari kupokea msaada kutoka kwa Allaah. Kitendo hichi cha Jibriyl kumuonyesha haja Ibraahiym ni dalili inayoonyesha kuwa inafaa kumtaka msaada na uokozi asiyekuwa Allaah. Kwa sababu Jibriyl alijionyesha na kama ingelikuwa ni jambo lililokatazwa basi Jibriyl asingelijionyesha. Ndipo akawajibu watu hawa kwa kuwaambia kwamba huu ni ujinga mkubwa. Kwa sababu Jibriyl ni Malaika mkubwa ambaye amepewa nguvu nyingi na Allaah. Amejionyesha kwake ili aweze kumsaidia kwa kitu ambacho ana uwezo nacho ambapo Ibraahiym akamjibu kwamba hana haja kutoka kwake na kwamba ana haja kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Iwapo Allaah angelimwamrisha Jibriyl kumchukua Ibraahiym kuelekea upande wa juu mbinguni, sehemu ya mbali au kuzima moto angelifanya hivo. Kwani yeye ni mwenye nguvu na ni mwaminifu (´alayhis-Swalaah was-Salaam):

إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ ذِي قُوَّةٍ عِندَ ذِي الْعَرْشِ مَكِينٍ مُّطَاعٍ ثَمَّ أَمِينٍ

“Hakika hii bila shaka ni kauli ya Mjumbe mtukufu. Mwenye nguvu na cheo kitukufu kwa Mwenye kumiliki ‘Arshi. Anayetiiwa mwaminifu.”[1]

Huyu ni Jibriyl (´alayhis-Swalaah was-Salaam). Huyu ndiye ambaye kumesemwa juu yake:

عَلَّمَهُ شَدِيدُ الْقُوَىٰ ذُو مِرَّةٍ فَاسْتَوَىٰ

“Amemfunza mwenye nguvu madhubuti. Mwenye muonekano mzuri na akalingamana sawasawa.”[2]

Mfano wa tukio hili ni kama mtu fakiri ambaye amejitokeza kwake ambaye ana mali nyingi na kumuuliza kama yuko na haja amsaidie na kama anataka mavazi, pesa au chakula, ambapo yule fakiri akamjibu kwamba hamuhitajii yeye na kwamba haja yake ataitatua kwa njia nyingine. Je, kuna ubaya katika jambo hili? Hakuna ubaya wowote. Shirki iliobainishwa ndani ya Qur-aan ni kile kitendo cha mtu kuwaendea wafu, miti, mawe, nyota, sanamu au viumbe vilivyoko mbali kama majini – pasi na sababu zenye kuhisiwa – na kuyaomba msaada, kuyawekea nadhiri na kuyaomba uokozi. Haya ndio yaliyobainishwa na Qur-aan kwamba ni shirki na kwamba lililo la wajibu kwa muumini ni yeye kujichunga nayo. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[3]

يُولِجُ اللَّيْلَ فِي النَّهَارِ وَيُولِجُ النَّهَارَ فِي اللَّيْلِ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ كُلٌّ يَجْرِي لِأَجَلٍ مُّسَمًّى ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ لَهُ الْمُلْكُ ۚ وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ مَا يَمْلِكُونَ مِن قِطْمِيرٍ إِن تَدْعُوهُمْ لَا يَسْمَعُوا دُعَاءَكُمْ وَلَوْ سَمِعُوا مَا اسْتَجَابُوا لَكُمْ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُونَ بِشِرْكِكُمْ ۚ وَلَا يُنَبِّئُكَ مِثْلُ خَبِيرٍ

“Anauingiza usiku ndani ya mchana na anauingiza mchana ndani ya usiku na anaitisha jua na mwezi; kila kimoja kinakwenda hadi muda maalum uliokadiriwa. Huyo ndiye Allaah, Mola wenu, ufalme ni Wake pekee.  Wale mnaowaomba badala Yake hawamiliki hata kijiwavu cha kokwa ya tende. Mkiwaomba, hawasikii maombi yenu, na hata wakisikia, hawatakuitikieni na siku ya Qiyaamah watakanusha ushirikina wenu na wala hakuna atakayekujulisha vyema kama Mwenye khabari zote.”[4]

Allaah (Subhaanah) ametahadharisha kutokamana na yale yanayofanywa na washirikina pamoja na masanamu na mizimu yao na akaeleza kuwa masanamu na mizimi hao haimiliki chochote na kwamba ufalme ni kwa Allaah pekee. Yeye (Jalla wa ´Alaa) ndiye anayeendesha ulimwengu.

[1] 81:19-21

[2] 53:05-06

[3] 72:18

[4] 35:13-14

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 126-129
  • Imechapishwa: 27/10/2021