33. Msimamo wa Maswahabah juu ya kufasiri Qur-aan

Kwa sababu hii wengi katika Salaf waliona uzito kufasiri jambo yale wasiyokuwa na elimu nayo. Kama ilivyosimuliwa Shu´bah Sulaymaan, kutoka kwa ´Abdullaah bin Murrah, kutoka kwa Abu Ma´mar, ambaye amesimulia kwamba Abu Bakr as-Swiddiyq amesema:

“Ni ardhi gani itakayobeba mwili wangu na ni mbingu gani itakayoniwekea kivuli ikiwa nitasema juu ya Kitabu cha Allaah yale nisiyoyajua?”[1]

Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam amesema: Muhammad bin Yaziyd ametuhadithia, kutoka kwa al-´Awwaam bin Hawshab, kutoka kwa Ibraahiym at-Taymiy, aliyesimulia kwamba Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) aliulizwa juu ya maneno Yake (Ta´ala):

وَفَاكِهَةً وَأَبًّا

”… na matunda na malisho ya wanyama… ”[2]

Akajibu: “Ni mbingu gani itakayonifunika na ardhi gani itakayobeba mwili wangu ikiwa nitasema juu ya Kitabu cha Allaah yale nisiyoyajua?”[3]

Cheni ya wapokezi ni yenye kukatika.

Abu ´Ubayd amesema tena: Yaziyd ametuhadithia, kutoka kwa Humayd, kutoka kwa Anas, aliyesimulia:

”´Umar bin al-Khattwaab alisimama juu ya mimbari na kusoma:

وَفَاكِهَةً وَأَبًّا

”… na matunda na malisho ya wanyama… ”[4]

Kisha akasema: ”Tumejua ni nini maana ya matunda, lakini mnajua ni nini maana ya nyasi? Halafu akajirejea mwenyewe na kusema: ”Huku ni kujikalifisha, ee ´Umar!”[5]

´Abd bin Humayd amesema: Sulaymaan bin Harb ametuhadithia: Hammaad bin Zayd ametuhadithia, kutoka kwa Thaabit, kutoka kwa Anas, ambaye amesema:

”Tulikuwa kwa ´Umar bin al-Khattwaab. Alikuwa amevaa kanzu yenye viraka vinne. Kisha akasoma:

وَفَاكِهَةً وَأَبًّا

”… na matunda na malisho ya wanyama… ”[6]

Akasema: ”Nyasi ni nini?” Kisha akasema: ”Huku ni kujikalifisha. Unadhurika nini usipojua ni kitu gani?”

Haya yote yanaweza kufasiriwa kwamba wao wawili (Radhiya Allaahu ´anhumaa) walitaka kutambulisha ni nini nyasi. Venginevyo wote walikuwa wanajua kuwa nyasi ni mimea inayoota ardhini, kwa sababu amesema (Ta´ala) :

فَأَنبَتْنَا فِيهَا حَبًّا وَعِنَبًا وَقَضْبًا وَزَيْتُونًا وَنَخْلًا وَحَدَائِقَ غُلْبًا وَفَاكِهَةً وَأَبًّا

”… Tukaotesha humo nafaka, na mizabibu na mimea ya mboga, na mizaituni na mitende, na mabustani yaliyositawi na kusongamana na matunda na malisho ya wanyama.”[7]

Ibn Jariyr amesema: Ya´quub bin Ibraahiym ametuhadithia: Ibn ´Ulayyah ametuhadithia, kutoka kwa Ayyuub, kutoka kwa Ibn Abiy Mulaykah, ambaye ameeleza:

”Ibn ´Abbaas aliulizwa kuhusu Aayah ambayo kama mmoja wenu angeulizwa, basi angeijibu. Lakini akakataa kujibu.”[8]

Cheni yake ya wapokezi ni Swahiyh.

Abu ´Ubayd amesema: Ismaa´iyl bin Ibraahiym ametuhadithia, kutoka kwa Ayyuub, kutoka kwa Ibn Abiy Mulaykah, ambaye ameeleza:

Bwana mmoja alimuuliza Ibn ´Abbaas kuhusiana na maneno Yake:

تَعْرُجُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ إِلَيْهِ فِي يَوْمٍ كَانَ مِقْدَارُهُ خَمْسِينَ أَلْفَ سَنَةٍ

”Malaika na Roho wanapanda Kwake katika siku kipimo chake ni sawa na miaka elfu khamsini.”[9]

Ibn ´Abbaas akamwambia: ”Ni nini maana ya:

”Siku kipimo chake ni sawa na miaka elfu khamsini” Bwana yule akasema: ”Nimekuuliza ili unihadithie.” Ibn ´Abbaas akamwambia: ”Hizo ni siku mbili zilizotajwa na Allaah ndani ya Kitabu Chake. Allaah ndiye mjuzi zaidi wa siku hizo.” Akachukizwa kusema juu ya Kitabu cha Allaah asiyoyajua.”

[1] Ibn Abiy Shaybah (30107), Jaamiy´-ul-Bayaan (1/58) na Jaamiy´ Bayaan-il-´Ilm (2/52).

[2] 80:31

[3] Fadhwaa-il-ul-Qur-aan, s. 227.

[4] 80:31

[5] Fadhwaa-il-ul-Qur-aan, s. 227.

[6] 80:31

[7] 80:27-31

[8] Jaamiy´-ul-Bayaan (1/62-63).

[9] 70:4

  • Muhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Muqaddimah fiy Usuwl-it-Tafsiyr, uk. 101-104
  • Imechapishwa: 14/04/2025