33. Mitihani inapelekea mtu kujirekebisha

Miongoni mwa faida za mitihani ni kuichukia dunia kutokana na shari zake na kujihimiza kutenda mema kwa ajili ya siku ya Qiyaamah. Yule anayewapoteza wapenzi wake anatambua kuwa na yeye atakutwa na jambo hilo. Muhammad bin al-Hasan amesema:

“Niliingia kwa Muhammad bin Muqaatil nikamwambia: “Ninasihi!” Akasema: “Fanya matendo! Kwani ukienda kamwe hutorudi. Watazame wafu; wamerudi?”

Masiku yetu yanaenda katika michezo

wakati madhambi yanaongezeka

Wako wapi wapenzi wetu na furaha yao?

Wamepotea na masiku ya maisha yao

Aidha mabalaa yanamlinda yule aliyefikwa na msiba kutokana na sifa zisizokuwa nzuri, ikiwa ni pamoja na kujikweza, kiburi, uovu, jeuri na majivuno. Ni wangapi waliojaribiwa ambao wametubia kikweli baada ya kupona! Ni wangapi waliojaribiwa ambao wamerudi kwa Allaah (Ta´ala) na kuboresha hali zao baada ya kuwa wamasikini! Ni wangapi waliojaribiwa ambao wamepata kutoka kwa Allaah sifa, rehema na uongofu Wake baada ya kuwakosa watoto wao na wakasubiri juu ya hukumu inayotekelezeka kwa waja Wake! Kwa njia hiyo inahakikiwa ile furaha inayokubalika katika Shari´ah juu ya msiba na yale yote yenye maana yake. Haihusiani na ile furaha ya kimaumbile, kwa sababu hapana shaka inakuwepo ile chuki ya kimaumbile. Mtu ambaye amepatwa na msiba halaumiwi juu ya kule kuhuzunika moyo wake na macho yake kutokwa na machozi. Hata hivyo kilichoharamishwa ni kule kufanya maombolezo na mfano wake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 117
  • Imechapishwa: 28/08/2023