Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, ni Kauli Yake (Ta´ala):

لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Hakika amekujieni Mtume anayetokana na nyinyi wenyewe, ni magumu juu yake yanayokutaabisheni, anakuhangaikieni, mwenye huruma mno na mapenzi tele kwa waumini.” (at-Tawbah 09:128)

Kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah maana yake ni kumtii katika yale aliyoamrisha, kumsadikisha kwa yale aliyoeleza, kujiepusha yale aliyokataza na kuyakemea na asiabudiwe Allaah isipokuwa kwa yale Aliyoyawekea Shari´ah.

MAELEZO

Shahaadah ya pili ni kuwa Muhammad ni Mtume wa Allaah. Dalili ya hilo ni maneno Yake (Ta´ala):

لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ

“Hakika amekujieni Mtume anayetokana na nyinyi wenyewe.”

Bi maana mnamtambua Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kuwa anatokamana na nyinyi na ni katika makabila matukufu kabisa anatokamana na Banuu Haashim:

عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ

“… ni magumu juu yake yanayokutaabisheni.”

Anahisi uzito kwa yale yanayokutieni uzito:

حَرِيصٌ عَلَيْكُم

“… anakuhangaikieni.”

Anapupia kuongoka kwenu na kukuokoeni kutokamana na Moto. Allaah (Ta´ala) amesema:

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّـهِ

“Muhammad ni Mtume wa Allaah.” (48:29)

Baada ya shahaadah hii ni juu ya mja kumtii (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika yale aliyoamrisha, kumsadikisha katika yale aliyokhabarisha, ajiepushe na yale aliyokataza na kukemea na asimuabudu Allaah isipokuwa kwa yale aliyoyawekea Shari´ah. Ni lazima kupatikane mambo haya mane:

1- Kumtii (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika yale aliyoamrisha kuhusu swalah, zakaah na mengineyo.

2- Kumsadikisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika yale aliyokhabarisha kuhusu Aakhirah, Pepo, Moto na mengineyo.

3- Kujiepusha na yale (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyokataza na kukemea kama vile uzinzi, ribaa na mengineyo yaliyokatazwa na Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

4- Allaah asiabudiwe isipokuwa kwa yale (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyoyawekea Shari´ah. Mja asizue katika dini kitu ambacho hakikuwekewa Shari´ah na Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu kitarudishwa.”[1]

“Atakayezua katika amri yetu hii yasiyokuwemo kitarudishwa.”[2]

Bi maana kitarudishwa.

[1] Muslim (1718).

[2] al-Bukhaariy (2697) na Muslim (1718).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 40-41
  • Imechapishwa: 12/01/2017