Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Kuwa na utambuzi wa kumtambua ndio maarifa kuu kabisa, kumwabudu ndio makusudio tukufu zaidi na kumfikia Yeye ndio lengo kubwa linalotakikana.

MAELEZO

Kutambua haki ya Allaah ya kuabudiwa pekee ndio lengo kuu kabisa. Ni kipi unachojua ikiwa humtambui Mola wako? Haitakikani kwa muislamu kutomtambua Mola wake. Yule asiyemtambua Mola wake ina maana vilevile hajui majina na sifa Zake na yale yote aliyojitambulisha Mwenyewe ndani ya Qur-aan na Sunnah. Isitoshe kujua peke yake haitoshi. Ni lazima pia kufanya ´ibaadah. Yule anayemjua Mola wake ni lazima vilevile amwabudu. Baadhi ya Suufiyyah wanasema kuwa yule ambaye anamtambua Mola wake basi hahitaji kujishughulisha na ´ibaadah kwa sababu eti tayari ameshafika kwa Allaah. Hili ni batili. Ni lazima yapatikane mambo mawili. Aidha kumtambua Allaah haina maana ya kuwa na utambuzi juu ya dhati Yake pasi na majina na sifa Zake. Kwa sababu hakuna yeyote anayejua dhati Yake isipokuwa Yeye mwenyewe. Namna ya majina na sifa Zake hakuna anayejua isipokuwa Allaah. Lakini kinachotupasa ni kumtambua kupitia yale majina na sifa Zake zilizothibitishwa kwa kujua maana yake na kumwabudu kwayo pasi na kupekua namna yake au dhati ya Mola (Subhaanahu wa Ta´ala). Hakuna yeyote awezaye kuifikia elimu hiyo – Allaah pekee ndiye anayeijua:

يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يُحِيطُونَ بِهِ عِلْمًا

“Anajua yale yaliyoko mbele yao na yale yaliyoko nyuma yao na hawawezi kumzunguka kwa kumtambua.”[1]

Hawawezi kumzunguka Mola (Subhaanahu wa Ta´ala) kiujuzi.

[1] 20:110

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 64-65
  • Imechapishwa: 04/08/2024