Mwili mzima wa mwanamke ni uchi. Hilo ni kutokana na maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwanamke ni uchi. Anapotoka, basi mwanamke humvizia.”

Ameipokea at-Tirmidhiy (1173) kupitia kwa ´Abdullaah bin Mas´uud. at-Tirmidhiy amesema: ”Hadiyth hii ni nzuri, Swahiyh na ngeni.” Tazama ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (273).

Kwa hiyo ni wajibu kwa mwanamke kufunika mwili wake wote, kukiwemo uso wake, mbele ya wanaume wasiokuwa maharimu zake. Shaykh wetu Muhammad al-Amiyn ash-Shanqiytwiy (Rahimahu Allaah) amesema katika kitabu chake ”Adhwhaa-’ul-Bayaan” katika mnasaba wa Suurah ”al-Ahzaab” (6/596) kuhusu Hadiyth hii:

“Kilichokuja ndani yake ya kwamba mwanamke ni uchi kinafahamisha uwajibu wa Hijaab, kwa kuwa ni lazima kufunika kila kitu kinachoitwa ´uchi´.”

Shaykh wetu pia ametaja (6/585–586) kuwa hukumu ya kufunika uso kwa wake wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni jambo ambalo wanazuoni wote wameafikiana juu yake na kwamba Aayah zilizoteremshwa kuhusu wao juu ya Hijaab zinajumuisha dalili mbili zinazothibitisha kuwa hukumu hiyo siyo maalum kwao tu, bali ni kwao pamoja na wanawake wengine wa ummah:

1 – Sababu ya wao kuamrishwa Hijaab kwa maneno Yake Allaah (Ta´ala):

ذَٰلِكُمْ أَطْهَرُ لِقُلُوبِكُمْ وَقُلُوبِهِنَّ

“Hivyo ni utwaharifu zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao.”[1]

Hilo ni kwa kuwa kama imesemwa hivyo kuhusu wake wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), pamoja na heshima waliyopewa na Allaah ya usafi na kutokuwa na tuhuma, basi wanawake wengine wa ummah ambao hawakupata heshima kama hiyo ni zaidi ya kuwa na haja ya Hijaab.

2 – Ni katika maneno Yake Allaah (´Azza wa Jall):

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاء الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّا

“Ee Nabii! Waambie wake zako na mabinti zako – na wanawake wa waumini – wajiteremshie Jilbaab zao.”[2]

Kwa sababu amri ya kujifunika kwa jilbaab ililetwa kwa wake wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), pia imeletwa kwa wasichana zake na wanawake wa waumini. Hii inafahamisha kuwa hukumu haikuhusiana na wake wa Mtume peke yao, bali pia inawahusu wanawake wengine. Kisha akabainisha (Rahimahu Allaah) ya kwamba ingelikuwa hukumu hiyo ni maalum kwa wake wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa namna ya ulazima, basi wao ni kielelezo bora kwa wanawake wengine. Akasema (6/592):

“Ukishajua kwa yale tuliyotaja kuwa hukumu ya Aayah ya Hijaab ni ya jumla na kwamba Aayah nyingine pamoja nayo zinathibitisha kwamba inawajibika mwanamke kufunika mwili wake wote mbele ya wanaume wasio maharimu, basi utajua kuwa Qur-aan imejulisha Hijaab. Na hata kama tutakadiria ya kwamba Aayah ya Hijaab ni maalum kwa wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi hapana shaka kuwa wao ni mfano mwema kwa wanawake wa Kiislamu katika adabu tukufu zinazotakiwa kwa usafi kamili na kujiepusha na uchafu wa tuhuma. Basi anayejitahidi kuwazuia wanawake wa Kiislamu – kama vile walinganizi wa leo wanaoita kukaa uchi, kuonyesha mapambo na kuchanganyika – dhidi ya kuwafuata wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika adabu hii ya mbinguni yenye kuhifadhi heshima na usafi dhidi ya uchafu wa tuhuma, basi huyo anawalaghai ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), mwenye maradhi moyoni kama unavyoona.”

Miongoni mwa dalili zilizo wazi zaidi kutoka katika Sunnah kuhusu uwajibu wa mwanamke kufunika uso wake mbele ya wanaume wasiokuwa maharimu ni yale yaliyokuja ndani yake kwamba wanawake walikuwa wakifunika miguu yao. ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayevuta vazi lake kwa kiburi, Allaah hatamwangalia siku ya Qiyaamah.” Umm Salamah akasema: “Itakuwaje basi wanawake wavaavyo nguo zenye mikia mirefu?” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Waachilie chini kiasi cha shibiri” Akasema: “Basi miguu yao itaonekana.” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Waachilie kiasi cha dhiraa na wasizidishe zaidi ya hapo.”

Imepokelewa na watunzi wa Sunan na wengineo. at-Tirmidhiy (1731) amesema: ”Hadiyth hii ni nzuri na Swahiyh.”

Basi kuja kwa Shari´ah kwa amri ya wanawake kufunika miguu yao kunafahamisha wazi ya kwamba kufunika uso ni wajibu, kwa kuwa uso ndio mahali pa fitina na uzuri wa mwanamke. Hivyo kufunika uso kunastahiki zaidi kuliko miguu.

Mwanamke muungwana anaposwali anafunika mwili wake wote isipokuwa uso wake. Hili alilotaja Shaykh (Rahimahu Allaah) amelinasibisha katika ”al-Mughniy” (2/326) kwa madhehebu ya Imaam Ahmad na akaitajia pia riwaya nyingine inayoruhusu kufunua viganja vya mikono na akainasibisha kwa Maalik na ash-Shaafi´iy. Pia ameinasibisha kwa Abu Haniyfah kuwa inajuzu kufunua miguu pamoja na uso na mikono.

[1] 33:53

[2] 33:59

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 33-37
  • Imechapishwa: 27/05/2026