Tumerudi katika kufasiri Hadiyth ya al-Haarith inayozungumzia mambo yanayomkinga mja dhidi ya adui yake. Maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Na Allaah amekuamrisha kufunga, kwani mfano wake ni kama mtu aliye kati ya kundi la watu akiwa na mfuko wa harufu nzuri ya miski; basi wote wanapendezwa na harufu yake au wanapendezwa nayo. Hakika harufu ya mtu anayefunga ni nzuri zaidi mbele ya Allaah kuliko harufu ya miski.”

Hakika amefananisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) jambo hili na mtu anayebeba mfuko wenye miski kwa sababu mfuko huu huwa umefichwa na macho ya watu na umehifadhiwa chini ya mavazi yake kama ilivyo kawaida ya mbeba miski. Vivyo hivyo mfungaji swawm yake imefichika na macho ya viumbe. Hisia zao haziwezi kuiona.

Mfungaji wa kweli ni yule ambaye viungo vyake vimehifadhiwa na madhambi, ulimi wake kusema uongo, maneno machafu, ushahidi wa uongo, tumbo lake limehifadhiwa na chakula na kinywaji na tupu yake imehifadhiwa na matamanio ya kijinsia. Basi akizungumza husema maneno yasiyoharibu swawm yake. Akitenda hatendi matendo yanayoharibu swawm yake. Basi maneno yake yote huwa na manufaa na yanaleta kheri. Vivyo hivyo kuhusu matendo yake. Hii ni mfano wa harufu nzuri anayoinusa mtu anayekaa karibu na mbeba miski. Hali kadhalika anayekaa karibu na mfungaji hunufaika na kikao chake naye na huwa salama dhidi ya uongo, ushahidi wa uongo, uovu na dhuluma. Hii ndiyo swawm iliyowekwa katika Shari´ah, siyo tu kujizuilia na chakula na kinywaji. Imekuja katika Hadiyth Swahiyh:

“Yeyote asiyeacha maneo ya uongo, kuyatendea kazi na ujinga, basi Allaah hana haja na yeye kuacha chakula chake na kinywaji chake.”[1]

Imekuja katika Hadiyth nyingine:

“Huenda mfungaji asiambulie chochote kutoka kwa swawm yake isipokuwa njaa na kiu.”[2]

Kwa hiyo swawm ni kule kujizuilia viungo dhidi ya madhambi na kujizuilia tumbo dhidi ya chakula na kinywaji. Kama vile chakula na kinywaji vinavunja swawm na kuibatilisha, vivyo hivyo madhambi huvunja thawabu zake na kuharibu matunda yake, hadi inakuwa kama mtu ambaye hakufunga kabisa.

[1] al-Bukhaariy (6057).

[2] an-Nasaa’iy (3236-3237), Ibn Maajah (1690) na Ahmad (3/379). Nzuri na Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (1083).

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 57-58
  • Imechapishwa: 09/08/2025