Hayo yote yamepigiwa mfano na nyumba tatu. Nyumba moja ni ya mfalme na ndani yake kuna hazina zake, akiba zake na vito vyake vya thamani. Nyumba nyingine ni ya mtumwa na ndani yake kuna hazina na akiba za mtumwa, lakini si vito wala akiba za mfalme. Nyumba nyingine ni tupu, haina kitu kabisa. Basi akaja mwizi kutaka kuiba kutoka katika mojawapo ya hizo nyumba. Je, ataiba katika nyumba ipi? Ukisema aibe kwenye nyumba iliyo tupu, hiyo haiwezekani kwa sababu nyumba hiyo haina chochote cha kuibwa.

Na ukisema aibe kutoka katika nyumba ya mfalme, hilo pia ni jambo lisilowezekana kabisa. Kwa sababu ina walinzi, waangalizi na hifadhi ambayo mwizi hawezi kuikaribia. Vipi atakaribia ilihali mlinzi wake ni mfalme mwenyewe? Vipi mwizi aweze kufika karibu na wakati imezungukwa na walinzi na askari? Hakubaki mwizi isipokuwa kuishambulia nyumba ya tatu na hiyo ndiyo anayoiandama kwa mashambulizi. Mwenye akili atafakari mfano huu vizuri sana na auweke juu ya hali ya nyoyo, kwa sababu nyoyo ziko katika muelekeo huu.

Kwa hiyo moyo ambao hauna kheri yoyote kabisa, nao ni moyo wa kafiri na mnafiki, hiyo ni nyumba ya shaytwaan. Tayari amejihakikishia kuwa ni yake na ameifanya maskani na makazi yake. Basi nini ataiba humo na hali ndani yake kuna hazina zake, akiba zake, mashaka, taswira za kupotea na wasiwasi wake?

Moyo ambao umejaa utukufu wa Allaah (´Azza wa Jall), ukuu, mapenzi, kumchunga na haya kutoka Kwake. Ni shaytwaan gani ataweza kuthubutu kuukaribia moyo huu? Na kama atataka kuiba kitu humo, basi atapata nini? Mwisho wa yote ni kwamba anafaulu kwa ghafla katika wakati wa kutomakinika kwa mja au kughafilika kwake, jambo ambalo haliwezi kuepukwa kwa kuwa ni mwanadamu na hukumu za ubinadamu zinampata kama kughafilika, kusahau, kupotea na kushindwa kwa maumbile. Imesemekana kwamba Wahb bin Munabbih (Rahimahu Allaah) alinukuu ndani ya kitabu cha kiungu kinachosema:

”Sikai katika nyumba na wala hazinitoshi. Ni kitu gani chenye kuweza kunitosha ilihali mbingu zimejaa mahali Pangu pa kuwekea miguu? Lakini Niko katika moyo wa yule mwenye mapenzi ya kweli ambaye ameacha kila kitu kisichokuwa Mimi.”

Hii ndio maana ya masimulizi mengine yanayosema:

”Mbingu Zangu wala ardhi Yangu hazikunitosha, lakini moyo wa mja Wangu muumini ndio umenitosha.”

Moyo ambao ndani yake kuna kumpwekesha Allaah (Ta´ala), maarifa Yake, mapenzi Yake, imani Kwake na kusadiki ahadi na matishio Yake.  Ndani yake pia kuna matamanio ya nafsi, tabia zake, mambo yanayomvutia na maumbile yake. Wakati fulani moyo wake unaelekea wito wa imani, maarifa na mapenzi kwa Allaah (Ta´ala) na kumtakasa Yeye peke Yake. wakati mwingine moyo wake unaelekea wito wa shaytwaan, matamanio na maumbile. Shaytwaan anakuwa na matumaini kwa moyo kama huu. Ndani yake kuna mapambano na vita – na Allaah humpa ushindi amtakaye:

وَمَا النَّصْرُ إِلَّا مِنْ عِندِ اللَّـهِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ

”Hakuna ushindi isipokuwa kutoka kwa Allaah Mwenye nguvu Aliyeshinda, Mwenye hekima.”[1]

Shaytwaan hawezi kutawala moyo huu isipokuwa kwa silaha zake alizonazo. Huingia kwake na kuzikuta silaha hizo zipo tayari ambapo akazichukua na kuushambulia moyo. Silaha hizo ni matamanio, mashaka, fikira potofu na matarajio ya uongo. Silaha hizi ziko ndani ya moyo. Basi shaytwaan huingia na kuzikuta tayari ambapo akazichukua na kuushambulia moyo nazo. Ikiwa mja atakuwa na imani yenye nguvu inayokabiliana na silaha hizo na kuzizidi nguvu, basi humshinda shaytwaan. Kama sivyo, basi ushindi unakuwa kwa adui yake dhidi yake. Akimpa ruhusa adui yake, akamfungulia mlango wa nyumba yake, akamuingiza ndani na akampa uwezo wa kutumia silaha ya kumshambulia nayo, basi yeye ndiye mwenye kusimangwa:

Jilalamikie nafsi yako wala usilalamikie wanyama wa kubebea –

na kufa kwa huzuni, kwa sababu huna udhuru

[1] 03:126

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 53-56
  • Imechapishwa: 09/08/2025