127 – ´Aliy bin Hujr ametukhabarisha: Ismaa´iyl ametukhabarisha: Humayd ametuhadithia, kutoka kwa Anas, ambaye ameeleza:

“Mama yake Haarithah alikwenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya Haarithah kupigwa na mshale siku ya Badr na akafa, akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Hakika unajua nafasi anayo Haarithah moyoni mwangu. Sitamlilia ikiwa yuko Peponi, lakini vinginevyo utaona ninachofanya.” Akasema: “Je, una wazimu? Je, Peponi ni moja tu? Pepo ni nyingi, naye yuko ile Pepo ya juu kabisa.”[1]

128 – Muhammad bin Haatim bin Nu´aym ametukhabarisha: Hibbaan ametukhabarisha: ´Abdullaah ametukhabarisha, kutoka kwa Sulaymaan bin al-Mughiyrah, kutoka kwa Thaabit, kutoka kwa Anas, ambaye amesema:

“Siku ya Badr, mtoto wa shangazi yangu HAarithah alikwenda kutazama na sio kupigana. Akapatwa na mshale na akafa. Shangazi yangu, yaani mama yake akaenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na akasema: “Mtume wa Allaah! Ikiwa mwanangu Haarithah yumo Peponi, nitafanya subira na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah. Vinginevyo utaona ninachofanya.” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema: “ Ee Umm Harithah, Pepo ni nyingi, na Harithah yuko katika ile Pepo ya juu kabisa.”

129 – Muhammad bin Raafiy´ ametukhabarisha: ´Abdur-Razzaaq ametukhabarisha: Ma´mar ametukhabarisha … Pia Ishaaq bin Ibraahiym ametukhabarisha: ´Abdur-Razzaaq ametukhabarisha: Ma´mar ametukhabarisha, kutoka kwa az-Zuhriy, kutoka kwa ´Amrah, kutoka kwa ´Aaishah, kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye amesema:

“Nililala na kujiona nipo Peponi. Nikasikia sauti ikisomeka na kusema, “Ni nani huyo?” Ikasemwa: “Kisomo cha Haarithah bin an-Nu’maan.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Huko ni kutenda wema. Huko ni kutenda wema. Huko ni kutenda wema.” Alikuwa ni miongoni mwa watu wanaowatendea sana mama zao.”[2]

Tamko ni la Ishaaq.

130 – Muhammad bin Naswr ametukhabarisha: Ayyuub bin Sulaymaan bin Bilaal ametukhabarisha: Abu Bakr ametuhadithia, kutoka kwa Sulaymaan, kutoka kwa Muhammad na Muusa: Ibn Shihaab ametukhabarisha, kutoka kwa Sa´iyd bin al-Musayyab, kutoka kwa Abu Hurayrah, aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nilipokuwa nikiota kwamba niko Peponi, nikasikia sauti ya mtu akisoma Qur-aaan na nikasema: “Ni nani huyo?” Wakasema: “Ni Haarithah bin an-Nu’maan. Huko ni kutenda wema. Huko ni kutenda wema. Huko ni kutenda wema.”

[1] al-Bukhaariy (6567).

[2] Ahmad (6/36) na al-Haakim (4/151), ambaye amesema kuwa ni Swahiyh kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy na Muslim.

  • Muhusika: Imaam Ahmad bin Shu´ayb an-Nasaa’iy (afk. 303)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwaa-il-us-Swahaabah, uk. 93-94
  • Imechapishwa: 15/09/2026