32. Basi huna lolote kabisa kuhusiana na Sunnah

160 – Haijuzu kwa mtu kusema kuwa fulani ni mtu wa Sunnah mpaka ajue kuwa amekusanya vipengele vyote vya Sunnah. Kwa hivyo hakusemi kwamba fulani ni mtu wa Sunnah mpaka akusanyikiwe na Sunnah yote.

161 – ´Abdullaah bin al-Mubaarak amesema:

“Msingi wa matamanio sabini na mbili ni matamanio mane. Kutoka katika matamanio haya manne ndio kumechipuka matamanio haya sabini na mbili: Qadariyyah, Murji-ah, Shiy´ah na Khawaarij.”[1]

Yule mwenye kuonelea kuwa Abu Bakr, kisha ´Umar, kisha ´Uthmaan na halafu ´Aliy wanakuja mbele ya Maswahabah wengine wote wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), asiwazungumzie wengine isipokuwa kwa kheri tupu na akawaombea du´aa nzuri, basi hana lolote kuhusiana na ´Aqiydah ya Shiy´ah.

Mwenye kusema kuwa imani ni maneno na vitendo na kwamba inazidi na kupungua, basi hana lolote kuhusiana na ´Aqiydah ya Murji-ah.

Ambaye atasema kuwa kunaswaliwa nyuma ya kila mwema na mwovu, jihaad itaendelea pamoja na kila mtawala, asionelei kufaa kufanya uasi dhidi ya mtawala kwa panga na akawaombea kutengemaa, basi hana lolote kuhusiana na ´Aqiydah ya Khawaarij.

Yule mwenye kusema kuwa makadirio yote kheri na shari yake yanatokana na Allaah (´Azza wa Jall), anampotosha na kumwongoza amtakaye, basi hana lolote kuhusiana na ´Aqiydah ya Qadariyyah. Huyo ni mtu wa Sunnah.

[1]  al-Ibaanah al-Kubraa (278) ya Ibn Battwah.

  • Mhusika: Imaam Abu Muhammad al-Hasan bin Khalaf al-Barbahaariy (kfk. 329)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh-us-Sunnah, uk. 132-133
  • Imechapishwa: 30/12/2024