Ahl-us-Sunnah wanaitakidi kuwa muumini ingawa atafanya madhambi mengi, ni mamoja madogo au makubwa, hakufuru kutokana nayo. Akiaga dunia katika hali hiyo kabla ya kutubia, wakati huohuo akafa juu ya upwekeshaji na kumtakasia nia Allaah, jambo lake liko kwa Allaah (´Azza wa Jall); akitaka atamsamehe na kumwingiza Peponi siku ya Qiyaamah hali ya kuwa ni mwenye kusalimika na mwenye kushinda bila ya kujaribiwa na Moto kutokana na aliyoyafanya na kuyatenda kisha yatamfuata yale madhambi na makosa mpaka siku ya Qiyaamah, na akitaka atamuadhibu Motoni kwa kipindi fulani kisha baadaye kumsamehe. Endapo atamuadhibu, basi hatomdumisha humo milele. Halafu atamwacha huru, kumtoa na kumwingiza ndani ya neema za makazi ya Milele. Mwalimu wetu Sahl bin Muhammad (Rahimahu Allaah) alikuwa akisema:

”Hata kama muumini mtenda dhambi atadhibiwa Motoni, hatotupwa ndani yake kama makafiri. Wala hatobaki humo kama makafiri. Wala hatokula maangamivu kama maangamivu ya makafiri.”

Maana yake ni kwamba kafiri ataburutwa Motoni kwa uso wake, ambapo atatupwa humo kwa kugeuzwa juu chini, akiwa amefungwa minyororo, kola za chuma, pingu na vitu vizito. Endapo muumini mtenda dhambi atajaribiwa Motoni, basi ataingia humo kama jinsi muhalifu anavyoingia jela duniani, bila ya kutupwa wala kugeuzwa juu chini. Kusema kuwa hatotupwa humo kama kafiri, maana yake ni kwamba kafiri mwili wake wote utachomwa. Kila pale ambapo itaungua ngozi yake, basi atabadilishiwa ngozi nyingine ili aonje adhabu ipasavyo. Hayo yamebainishwa na Allaah (Ta´ala) ndani ya Kitabu Chake pale aliposema:

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِنَا سَوْفَ نُصْلِيهِمْ نَارًا كُلَّمَا نَضِجَتْ جُلُودُهُم بَدَّلْنَاهُمْ جُلُودًا غَيْرَهَا لِيَذُوقُوا الْعَذَابَ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَزِيزًا حَكِيمًا

”Hakika wale waliokanusha Aayah Zetu, Tutawaingiza Motoni. Kila ngozi zao zitapowiva Tutawabadilishia ngozi nyingine ili waonje adhabu. Hakika Allaah daima ni Mwenye nguvu Asiyeshindika, Mwenye hekima.”[1]

Ama waumini, nyuso zao hazitochomwa Moto. Vile viungo vyao vya mwili walivyokuwa wakisujudia havitochomwa Moto. Kwani Allaah ameuharamishia Moto kuchoma vile viungo vya mwili wanavyosujudu kwavyo.

Kusema kwamba hawatobaki Motoni kama makafiri maana yake ni kwamba makafiri watadumishwa humo milele; kamwe hawatotoka. Allaah hatomwacha muumini mtenda dhambi yeyote kudumu humo milele.

Kusema kwamba hatokula maangamivu Motoni kama makafiri, maana yake ni kwamba makafiri watakata tamaa na rehema za Allaah na hawatokuwa na matarajio yoyote. Kuhusu waumini kamwe hawatokata tamaa na rehema za Allaah. Mafikio ya mwisho ya waumini wote ni Pepo, kwa sababu wameumbiwa kwayo na yenyewe imeumbiwa kwa ajili yao – fadhilah na neema kutoka kwa Allaah.

[1] 4:56

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 276-278
  • Imechapishwa: 19/12/2023