31. Kuifanya Qur-aan ni njia ya kujipatia riziki

Miongoni mwa mambo muhimu anayoyaamrishwa ni kujihadhari sana na kuifanya Qur-aan kuwa ni njia ya kujipatia riziki.  ´Abdur-Rahmaan bin Shibl (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Isomeni Qur-aan! Msile kwayo, msiipuuze na wala msichupe mipaka kwayo.”[1]

Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Isomeni Qur-aan kabla hawajaja watu watakaoisimamisha kama kusimamisha mshale; wataiharakisha wala hawatayachelewesha.”[2]

Ameipokea Abu Daawuud kupitia kwa Sahl bin Sa´d.

Maana yake ni kwamba wanaharakisha malipo yake ama kwa mali, kutaka kusikika na mfano wake.

Fudhwayl bin ´Amr (Rahimahu Allaah) amesema:

”Watu wawili miongoni mwa Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) waliingia msikitini. Imamu alipomaliza swalah, alisimama mtu akasoma Aayah kutoka Qur-aan kisha akaomba. Mtu mmoja akasema: ”Hakika sisi ni wa Allaah na Kwake tutarejea. Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema: ”Watakuja watu watakaomba kupitia Qur-aan. Yeyote atakayeomba kupitia Qur-aan msimpe.”

Cheni ya wapokezi ni yenye kukatika. Fudhwayl bin ´Amr hakusikia kutoka kwa Maswahabah.

Kuhusu kuchukua malipo kwa ajili ya kufundisha Qur-aan, wanazuoni wametofautiana katika hilo. Imaam Abu Sulaymaan al-Khattwaabiy ametaja kukataza kuchukua malipo kwa hilo kutoka kwa kikosi cha wanazuoni, ambapo miongoni mwao ni az-Zuhriy na Abu Haniyfah. Ametaja pia kwamba jopo la wanazuoni linalojuzisha ikiwa malipo hayakuwekwa kama sharti; akiwemo al-Hasan al-Baswriy, ash-Sha´biy na Ibn Siyriyn. ´Atwaa, Maalik, ash-Shaafi´iy na wengineo wameona kujuzu ikiwa ameweka sharti na akamwajiri kwa mkataba sahihi. Zimekuja Hadiyth Swahiyh zinazothibitisha kujuzu.

Wale waliojuzisha kitendo hicho wamejengea hoja kwa Hadiyth ya ´Ubaadah bin as-Swaamit:

”Alimfundisha mtu Qur-aan miongoni mwa watu wa Suffah, kisha akampa zawadi ya upinde, ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: ”Ukipenda kufungwa nao kitanzi cha moto basi ukubali.”[3]

Ameipokea Abu Daawuud na wengineo. Kuna masimulizi mengi mfano wa hayo kutoka kwa Salaf.

Wale waliojuzisha kitendo hicho wamejibu Hadiyth ya ´Ubaadah kwa njia mbili:

1 – Cheni ya wapokezi ina dosari.

2 – Alimfundisha kwa kujitolea yeye mwenyewe na hivyo hakustahiki chochote. Kisha akapewa zawadi kwa njia ya badala na hivyo haikujuzu kwake kuipokea, tofauti na yule anayefanya mkataba wa ajira kabla ya kufundisha – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[1] Ahmad (15529). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-ul-Jaamiy´” (1168).

[2] Ahmad (15308) na Abu Daawuud (830). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-ul-Jaamiy´” (1167).

[3] Abu Daawuud (3416). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (3416).

  • Muhusika: Imaam Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy (afk. 677)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tibyaan fiy Aadaabi Hamalat-il-Qur-aan, uk. 39-40
  • Imechapishwa: 26/08/2026