Sehemu yake imeshatangulia katika mlango uliotangulia. Miongoni mwa adabu zake ni kuwa katika hali iliyo kamilifu zaidi na tabia zilizo tukufu zaidi na ainyanyue nafsi yake mbali na kila jambo ambalo Qur-aan imekataza kwa ajili ya kuitukuza Qur-aan. Awe amejilinda na kipato cha chini, mwenye heshima ya nafsi, aliye juu ya madhalimu na wakali miongoni mwa watu wa dunia, mnyenyekevu kwa watu wema na wenye kheri na masikini. Awe mwenye unyenyekevu, mtulivu na mwenye heshima. ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Enyi watu wa Qur-aan, nyanyueni vichwa vyenu! Kwani njia imebainika kwenu. Shindaneni katika kheri na wala msiwe tegemezi kwa watu.”

´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Inampasa msomaji wa Qur-aan ajulikane kwa usiku wake wakati watu wamelala, mchana wake wakati watu wanakula, kwa huzuni yake wakati watu wanafurahi, kwa kulia kwake wakati watu wanacheka, kwa kunyamaza kwake wakati watu wanazungumza na kwa unyenyekevu wake wakati watu wanajivuna.”

al-Hasan bin ´Aliy (Rahimahu Allaah) amesema:

”Hakika waliokuwa kabla yenu waliiona Qur-aan kuwa ni barua kutoka kwa Mola wao; basi walikuwa wanaizingatia usiku na wanaichunguza mchana.”

al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw (Rahimahu Allaah) amesema:

”Inampasa msomaji wa Qur-aan asiwe na haja kwa yeyote miongoni mwa watawala au walio chini yao.”

Amesema tena:

”Msomaji wa Qur-aan ni mbebaji wa bendera ya Uislamu. Haifai acheze pamoja na wanaocheza, asisahau pamoja na wanaosahau na wala asizungumze upuuzi pamoja na wanaozungumza upuuzi kwa ajili ya kutukuza haki ya Qur-aan.”

  • Muhusika: Imaam Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy (afk. 677)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tibyaan fiy Aadaabi Hamalat-il-Qur-aan, uk. 38
  • Imechapishwa: 26/08/2026