31. Baadhi ya sifa mbaya mbaya wakati wa msiba

Katika Hadiyth zilizotajwa na zilizoharamisha kuna dalili tosha kwa yule mwenye kuzizingatia. Ni vipi sifa hizi mbaya zitakuwa sio za haramu ikiwa ni pamoja na kwamba zina kumkasirikia Mola (´Azza wa Jall) ambaye anafanya anachokitaka, anahukumu anavyotaka na ndiye mwenye kuwaendesha waja Wake ili baadhi yao wafe, wazame, waungue mpaka wafe na mengine katika hayo ambayo amekadiria na kupanga na kufanya yapitike. Haulizi kwa kile anachokifanya, lakini watu wataulizwa kwa yale waliyoyafanya. Kadhalika inahusiana na kuomboleza, kuchana nguo, kujipiga kwenye mshavu, kujichana usoni, kujikokota nywele, kutembea miguu peku, kuchora uso na mwili kwa rangi nyeusi, kujiombea umauti na maangamivu na maneno na matendo mengine ambayo dini imeharamisha na kuwakemea wenye kuyafanya. Matendo haya yanapingana na kuridhia na kuwa na subira. Yanaidhuru nafsi na mwili na hayabadilishi kitu ambacho Allaah kishakikadiria.

Nimepata khabari jinsi baadhi ya watu wanavyokuwa wagonjwa wanapofikiwa na khabari kuwa ndugu zao wamepatwa na msiba. Lau yule mwenye kusibiwa angelijisalimisha kwa Allaah na akamuachia jambo lake Yeye ambaye mambo yote yamo mkononi Mwake na akatambua kuwa furaha ya wanaadamu duniani na Aakhirah iko katika kuwafuata Mitume na kumfuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika yale aliyoamrisha na kukataza ikiwa ni pamoja vilevile na maneno na matendo haya yaliyoharamishwa, basi angelifikia furaha duniani na Aakhirah kwa kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa maneno na vitendo. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا

“Yale anayokupeni Mtume yachukueni, na yale anayokukatazeni, yaacheni.” (59:07)

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 53-54
  • Imechapishwa: 14/10/2016