30. Dalili kuhusu ujuu na kulingana kwa Allaah juu ya ´Arshi

Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah (Ta´ala) amesema:

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.” (20:05)

Imekuja namna hii sehemu saba. Sehemu ya kwanza ni katika ”al-A´raaf”:

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ

“Hakika Mola wenu ni Allaah ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ´Arshi.” (7:54)

Sehemu ya pili ni katika ”Yuunus”:

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ

“Hakika Mola wenu ni Allaah ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ‘Arshi.” (10:3)

Sehemu ya tatu ni katika ”ar-Ra´d”:

اللَّـهُ الَّذِي رَفَعَ السَّمَاوَاتِ بِغَيْرِ عَمَدٍ تَرَوْنَهَا ۖ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ

“Allaah ambaye ameziinua mbingu pasi na nguzo mnaziona kisha akalingana juu ya ‘Arshi.” (13:2)

Sehemu ya nne ni katika ”Twaa Haa”:

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.” (20:05)

Sehemu ya tano ni katika ”al-Furqaan”:

الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۚ الرَّحْمَـٰنُ فَاسْأَلْ بِهِ خَبِيرًا

”Ambaye ameumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake katika siku sita, kisha akalingana juu ya ‘Arshi; Mwingi wa rehema; basi ulizia kuhusu khabari Zake.”!” (25:59)

Sehemu ya sita ni katika ”as-Sajdah”:

اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ

“Allaah ambaye ameumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake ndani ya siku sita kisha akalingana juu ya ‘Arshi.” (32:4)

Sehemu ya saba ni katika ”al-Hadiyd”:

هُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَى عَلَى الْعَرْشِ

”Yeye ndiye aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ´Arshi.” (57:4)

MAELEZO

Kulingana Kwake (Subhaanahu wa Ta´ala) juu ya ´Arshi kumetajwa maeneo saba ndani ya Qur-aan; Twaa Haa, al-A´raaf, Yuunus, ar-Ra´d, al-Furqaan´, as-Sajdah na al-Hadiyd. Zote zimethibiti. Kulingana maana yake ni kuwa juu. Kulingana juu ya ´Arshi maana yake ni kwamba yuko juu ya ´Arshi. Yeye ndiye ambaye yuko juu ya viumbe Wake wote. ´Arshi ndio dari ya viumbe. Yeye Allaah (Subhaanah) yuko juu ya ´Arshi. Ni kulingana ambako kunalingana na utukufu Wake. Hakuna anayejua namna yake isipokuwa Yeye pekee (Subhaanahu wa Ta´ala). Wakati Imaam Maalik bin Anas (Rahimahu Allaah), ambaye alikuwa ni mwanachuoni mkubwa wa Madiynah katika wakati wake na mmoja katika maimamu wanne, alipoulizwa: “Ee Abu ´Abdillaah!

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”

Amelingana namna gani?” Akajibu: “Kulingana juu kunatambulika. Namna haitambuliki. Ni wajibu kuamini hilo na kuuliza juu ya hilo ni Bid´ah.” Kisha akaamrisha bwana huyo atolewe nje.”[1]

Vivyo hivyo ndivyo alivyosema Sufyaan ath-Thawriy, al-Awzaa´iy, Imaam Ahmad, Imaam ash-Shaafi´iy, Ishaaq bin Raahuuyah na maimamu wengine wa Uislamu. Maana ya kulingana inajulikana. Maana yake ni kuwa juu. Namna haijulikani. Kwa msemo mwingine hakuna anayejua namna alivyolingana isipokuwa Yeye pekee (Subhaanahu wa Ta´ala). Kuamini hilo ni wajibu, kwa sababu Allaah ndiye amejielezea Mwenyewe. Kuulizia namna ni Bid´ah iliyozuliwa na wanafalsafa kama vile Jahmiyyah, Mu´tazilah na wengineo.

[1] ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah, uk. 33, ya ad-Daarimiy, Sharh Usuwl I´tiqaad Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah (2/398) ya al-Laalakaa’iy, al-Asmaa’ was-Swifaat (867) ya al-Bayhaqiy na at-Tamhiyd (7/151) ya Ibn ´Abdil-Barr. Ibn Hajar  amesema:

”Cheni yake ya wapokezi ni nzuri.” (Fath-ul-Baariy (13/407))

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 42-43
  • Imechapishwa: 21/10/2024