29. Swalah ya mkusanyiko ni lazima kwa msafiri

Swali 29: Mtu akitaka kusafiri maeneo ya mbali ambayo yako mbali na makazi yake mwendo wa saa moja kwa ndege – je, inafaa kwake kukusanya na kufupisha swalah ilihali anakaa hotelini mwake au maeneo ya makazi yake? Je, inafaa kwake kula katika Ramadhaan[1]?

Jibu: Haifai kwa yeyote kufupisha swalah katika hali ya ukazi. Isipokuwa akiwa mgonjwa ambaye swawm ni ngumu kwake au msafiri katikati ya safari yake.

Kuhusu ambaye amekusudia kusafiri ilihali bado yuko katika mji wake haifai kwake kufupisha mpaka pale atakaposafiri na akayaacha majengo ya mji wake. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anapotaka kusafiri basi hafupishi mpaka pale anapoondoka kutoka katika mji. Hana ruhusa yeyote kuswali peke yake. Ni mamoja msafiri au mwenyeji maeneo ambapo kunaswaliwa swalah ya mkusanyiko. Bali ni lazima kwake kuswali na kukamilisha swalah pamoja na watu wengine. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayesikia wito na asiutikie basi hana swalah isipokuwa kutokana na udhuru.”[2]

Ameipokea Ibn Maajah, ad-Daaraqutwniy, Ibn Hibbaan na al-Haakim kwa cheni ya wapokezi wake inayoafikiana na sharti za Muslim.

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) aliulizwa:

“Ni upi udhuru?” Akasema: “Khofu au maradhi.”

Bwana mmoja kipofu alimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kusema: “Ee Mtume wa Allaah! Sina kiongozi wa kuniongoza msikitini. Je, ninayo ruhusa ya kuswali nyumbani kwangu?” Akamuuliza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Je, wasikia wito wa swalah?” Akasema: “Ndio.” Akasema: “Basi imewajibika.”[3]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nimetamani niamrishe kuswaliwe ambapo ikasimamishwa kisha nikamwamrisha mtu awaswalishe watu halafu nikaondoka na kikosi cha wanamme walio na vifurushi vya kuni kuwaendea watu ambao hawashuhudii swalah nikazichoma nyumba zao kwa moto.”[4]

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Anayetaka kukutana na Allaah kesho hali ya kuwa muislamu basi azihifadhi swalah hizi pindi zinaponadiwa. Hakika Allaah amemuwekea Nabii wenu njia za uongofu – nazo ni njia za uongofu. Endapo mtaswali majumbani mwenu kama anavoswali nyumbani kwake huyu anayebaki nyuma basi mtakuwa mmeiacha njia ya Mtume wenu. Mkiacha njia ya Mtume wenu basi mtapotea. Hakuna mtu anayejitwahirisha akaweka vizuri twahara yake kisha akaenda msikitini miongoni mwa misikiti hii isipokuwa Allaah atamwandikia jema moja, atamuinua ngazi na kumfutia kosa moja kwa kila hatua anayopiga. Tulikuwa tukiona hakuna anayeiacha [swalah ya mkusanyiko] isipokuwa ni mnafiki ambaye unatambulika unafiki wake au mgonjwa. Mtu alikuwa akibebwa kati ya watu wawili mpaka anasimamishwa katika safu.”[5]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Zipo Hadiyth nyingi zenye maana kama hii.

Kwa hiyo ni lazima kwa kila muislamu – ni mamoja msafiri au mkazi – aswali katika mkusanyiko na ahudhurie swalah muda wa kuwa anasikia wito wa swalah.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/39-41).

[2] Ibn Maajah (793).

[3] Muslim (653) na an-Nasaa´iy (850).

[4] al-Bukhaariy (6683) na Muslim (1041) na tamko ni lake.

[5] Muslim (1046).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Musaafir, uk. 43-46
  • Imechapishwa: 13/03/2022