29. Ngazi ya kwanza ya makadirio – ujuzi wa Allaah wa milele

Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

51 – Kwani Allaah (Ta´ala) amewaficha ujuzi wa makadirio viumbe Wake na akawakataza kujitahidi kuijua. Amesema (Ta´ala):

لَا يُسْأَلُ عَمَّا يَفْعَلُ وَهُمْ يُسْأَلُونَ

“Haulizwi kwa yale Anayoyafanya, lakini wao wataulizwa.”[1]

MAELEZO

Kutokana na ukamilifu wa hekima, rehema na uadilifu Wake, na si kwa sababu tu ya ufalme na uwezo Wake, kama anavodai Jahm na wafuasi wake. Hivo ndivo ilivyo katika maelezo. Rejea pia huko ambapo imethibitishwa kuwa msingi wa utumwa na imani umejengeka juu ya kujisalimisha na kuacha kuulizauliza juu ya pambanuzi za amri, makatazo na mambo ya Shari´ah. Ni jambo muhimu sana. Kama isingelikuwa kwa sababu ya ufinyu wa nafasi, basi ningeyanukuu hapa. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

”Kuamini makadirio kuna ngazi mbili na kila ngazi imebeba mambo mawili:

1 – Ngazi ya kwanza ni kuamini kuwa Allaah (Ta´ala) aliyajua kwa utambuzi Wake wa milele yale ambayo viumbe watayafanya, akazijua hali zao zote katika utiifu na maasi, riziki zao na muda wao wa kueshi. Kisha Allaah akayaandika makadirio hayo ya viumbe kwenye ubao Uliohifadhiwa:

“Kitu cha kwanza alichoumba Allaah ni kalamu. Akaiambia: “Andika!” Kukadiriwa yote yatayokuwepo hadi siku ya Qiyaamah.”[2]

Yale yaliyompata mwanadamu hayakuwa ya kumkosa na yale yaliyomkosa hayakuwa ya kumpata. Kalamu zimekauka na madaftari yamefungwa. Kama alivosema Allaah (Ta´ala):

أَلَمْ تَعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۗ إِنَّ ذَٰلِكَ فِي كِتَابٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Je, hujui kwamba Allaah anajua yale yote yaliyomo katika mbingu na ardhi? Hakika hayo yameandikwa katika Kitabu. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.”[3]

Makadirio haya ambayo yanafuatia ujuzi Wake (Subhaanah) yanakuwa maeneo mengi, kwa jumla na kwa upambanuzi. Ameandika kwenye ubao Uliohifadhiwa yale Anayoyataka, na wakati kipomoko kinapoumbwa na kabla ya kupuliziwa ndani yake roho, basi hutumiliziwa Malaika na akaamrishwa kumwandikia mambo manne: riziki yake, muda wake wa kueshi, matendo yake na kama atakuwa mla khasara au mwenye furaha. Ngazi hii inapingwa na Qadariyyah waliochupa mipaka hapo kale, na ni wachache ambao hii leo wanaipinga.

[1] 21:23

[2] Ahmad (5/317), Abu Daawuud (4700) na at-Tirmidhiy (2155). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwilaal-ul-Jannah” (1/48).

[3] 22:70

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 42-44
  • Imechapishwa: 25/09/2024