Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

al-´Irbaadhw bin Saariyah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitutolea mawaidha makali ambayo yalizitikisa nyoyo zetu na macho yetu yakatiririka machozi. Tukasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni kana kwamba ni mawaidha ya kutuaga; tuusie!” Akasema: “Ninakuusieni kumcha Allaah (´Azza wa Jall) na kusikiliza na kutii hata kama mtataliwa na mtumwa. Hakika yule atakayeishi katika nyinyi basi atakuja kuona tofauti nyingi. Hivyo basi, lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu watakasifu waongofu baada yangu. Shikamaneni nazo kwelikweli na ziumeni kwa magego. Tahadharini na mambo yenye kuzuliwa, kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”[1]

at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth ni Hasan na Swahiyh.”

Hudhayfah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kila ´ibaadah ambayo hawakuabudu kwayo Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi na nyinyi msiabudu kwayo. Wale wa mwanzo hawakuwapa wa mwisho la kusema. Mcheni Allaah, enyi wanazuoni, na shikeni njia ya waliokuwa kabla yenu.”[2]

 Ameipokea Abu Daawuud.

ad-Daarimiy amesema: “al-Hakam bin Mubaarak ametukhabarisha: ´Amr bin Yahyaa ametueleza: Nilimsikia baba yangu akieleza kutoka kwa baba yake ambaye amesema:

“Tulikuwa tukikaa nje ya mlango wa ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) kabla ya Fajr na anapotoka tunaenda naye mpaka msikitini. Siku moja akatujia Abu Muusa al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh) na kusema: “Abu ´Abdir-Rahmaan ameshakujieni?” Tukasema: “Hapana.” Akakaa na sisi mpaka alipotoka. Alipotoka sote tukasimama. Abu Muusa akamwambia: “Ee Abu ´Abdir-Rahmaan! Hivi karibuni nimeona msikitini kitu nimechokipinga na hakuna nilichoona isipokuwa ni kitu cha kheri tu.” Akasema: “Ni kipi?” Akasema: “Ukiishi utakiona. Msikitini nimewaona watu wamekaa mviringo wakisubiri swalah. Katika kila mviringo kuna mtu na mikononi mwao wana vijiwe vidogovidogo. Anasema: “Semeni: “Allaahu Akbar” mara mia”, wanafanya hivo. Kisha anasema: “Semeni: “Laa ilaaha illa Allaah” mara mia”, wanafanya hivo. Kisha anasema: “Semeni: “Subhaan Allaah” mara mia”, wanafanya hivo.” Akasema: “Uliwaambia nini?” Akasema: “Sikuwaambia kitu. Ninasubiri neno lako au amri yako.” Akasema: “Ungeliwaamrisha wahesabu madhambi yao na kuwadhamini kuwa hakuna chochote katika mema yao kitachopotea.” Halafu akaenda na tukafuatana naye. Alipofika katika mviringo mmoja miongoni mwa miviringo ile akasimama na kusema: “Nini haya ninayoona mnafanya?” Wakasema: “Ee Abu ´Abdir-Rahmaan! Ni vijiwe tu ambavyo tunafanya navyo Takbiyr, Tahliyl na Tasbiyh.” Akasema: “Hesabuni madhambi yenu. Mimi ninakudhaminini hakuna chochote katika mema yenu kitachopotea. Ee Ummah wa Muhammad! Ole wenu! Ni haraka iliyoje kuangamia kwenu! Hawa hapa Maswahabah wa Mtume wenu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) bado wamejaa, nguo zake hazijaharibika na chombo chake hakijapasuka. Ninaapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake ima nyinyi mkono katika dini bora kuliko dini ya Muhammad au mmefungua mlango wa upotevu.” Wakasema: “Ee Abu ´Abdir-Rahmaan! Hatukukusudia jengine isipokuwa kheri tu.” Akasema: “Ni wangapi wenye kuitaka kheri na hawaifikii! Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametueleza kuwa kutakuwepo watu wataoisoma Qur-aan pasi na kuvuka koo zao. Ninaapa kwa Allaah sijui pengine wengi wao ndio nyinyi wenyewe.” Kisha akatoka pale akenda zake.” ´Amr bin Salamah amesema: “Tuliona wengi katika wao wakishirikiana na Khawaarij siku ya Nahrawaan.”[3]

Allaah ndiye Mwenye kutakwa msaada na Mwenye kutegemewa. Swalah na salamu zimwendee kiongozi wetu Muhammad, familia yake na Maswahabah zake wote.

MAELEZO

Hapa kuna matahadharisho ya Bid´ah na kwamba ni lazima kwa waislamu kutahadhari nayo. Ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitawahadarisha wakati alipowatolea mawaidha, kama alivosema al-´Irbaadhw:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitutolea mawaidha makali ambayo yalizitikisa nyoyo zetu na macho yetu yakatiririka machozi. Tukasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni kana kwamba ni mawaidha ya kutuaga; tuusie!” Akasema: “Ninakuusieni kumcha Allaah (´Azza wa Jall) na kusikiliza na kutii – yaani watawala – hata kama mtataliwa na mtumwa. Hakika yule atakayeishi katika nyinyi basi atakuja kuona tofauti nyingi. Hivyo basi, lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu watakasifu waongofu baada yangu. Shikamaneni nazo kwelikweli na ziumeni kwa magego. Tahadharini na mambo yenye kuzuliwa, kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”

Ni lazima kwa waislamu kushikamana na yale ambayo Allaah amewawekea waja Wake na atahadhari na yale ambayo watu wamewazulia watu katika Bid´ah. Kwa ajili hii Hudhayfah amesema:

“Kila ´ibaadah ambayo hawakuabudu kwayo Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi na nyinyi msiabudu kwayo. Wale wa mwanzo hawakuwapa wa mwisho la kusema. Mcheni Allaah, enyi wanazuoni, na shikeni njia ya waliokuwa kabla yenu.”

Maswahah wamebainisha na wakamuuliza Mtume wao kuhusu kila kitu. Kwa hivyo ni lazima kuwaigiliza wao na kufuata njia yao.

Wakati ´Abdullaah bin Mas´uud alipowaona watu msikiti vikao ambapo kuna mmoja anawaambia waseme ”Subhaan Allaah” na wahesabu idadi fulani kwa vijiwe, ndipo akasema:

”Ima nyinyi mkono katika dini bora kuliko dini ya Muhammad au mmefungua mlango wa upotevu. Hesabuni madhambi yenu. Mimi ninakudhaminini hakuna chochote katika mema yenu kitachopotea.”

Hizi ni miongoni mwa Bid´ah na kufarikiana vikundivikundi. Kilicho cha wajibu ni kupeana nasaha na kunukuu yale aliyosema Allaah na Mtume Wake. Mambo yanatakiwa yawe namna hii. Ama kuweka vikao vya dhikr na kudhikiri kwa vijiwe ambapo kuna mmoja anawaambia wengine wahesabu idadi maalum, haya ni miongoni mwa mambo yaliyozuliwa na watu katika Bid´ah. Kwa ajili hii amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Khutbah:

”Amma ba´d, hakika mazungumzo bora ni Kitabu cha Allaah, uongofu bora kabisa ni wa Muhammad, uovu wa mambo ni yale yaliyozuliwa na kila Bid´ah ni upotevu.”[4]

Zile ´ibaadah zilizozuliwa na watu ndio Bid´ah. Bid´ah inakuwa katika mambo ya ´ibaadah. Yale ambayo watu wanajikurubisha kwayo miongoni mwa mambo ambayo hayakuwekwa katika Shari´ah ndio ambayo huitwa kuwa ni Bid´ah. Ni lazima kutahadhari nayo na hakuna upambanuzi. Kila Bid´ah ni upotevu.

Kuhusu maneno ya baadhi ya watu kwamba Bid´ah inagawanyika mafungu matano ni ya kimakosa. Sahihi ni kwamba kila Bid´ah ni upotevu . Bid´ah ni ile ´ibaadah ambayo mtu anajikurubisha miongoni mwa mambo ambayo Allaah hayakuweka katika Shari´ah. Haya ndio ambayo huitwa kuwa ni ´Bid´ah`. Ni kama mfano wa yale yaliyofanywa na watu hawa katika zama za Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh). Ni kama mfano wa uzushi wa kusherehekea mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kuyajengea makaburi, kujenga misikiti makaburini, kuyaweka chokaa makaburi na kuandika juu yake. Yote haya ni miongoni mwa mambo yaliyozuliwa na watu katika aina za Bid´ah.

Kwa hivyo ni lazima kutahadhari na mambo hayo. Muumini anatakiwa kujifungamanisha na yale ambayo Allaah ameyaweka katika Shair´ah na yale ambayo walipita juu yake Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika mambo ya ´ibaadah. Mtu anatakiwa ajichunge na kuzidisha katika ambayo Allaah (Jalla wa ´Alaa) ameyaweka katika Shari´ah. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

“Leo Nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio dini yenu.” (05:03)

Allaah amekamilisha dini. Kwa hivyo hana ruhusa yeyote kuzidisha. Tunamuomba Allaah msamaha na salama.

Swalah na amani zimwendee Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

[1] Abu Daawuud (4607), at-Tirmidhiy (2676) na Ibn Maajah (34). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (2455).

[2] Ibn-ul-Mubaarak katika ”az-Zuhd”, uk. 16, al-Marwaziy katika ”as-Sunnah” (1/30) na Ibn Abiy ´Aasim katika ”as-Sunnah” (1/90).

[3] ad-Daarimiy (204), Bahshal katika ”Taariykh Waaswit” na al-Khatwiyb al-Baghdaadiy katika ”Taariykh Baghdaad” (12/162).

[4] Muslim (867).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Fadhwl-il-Islaam, uk. 52-55
  • Imechapishwa: 12/11/2020