28. Yule anayejipinda kuitafuta Aakhirah basi hupata pia dunia

163 – Muhammad bin Abiy Bakr al-Maqdamiy ametukhabarisha: Yahyaa bin Sa´iyd al-Qattaan ametukhabarisha: Shu´bah ametukhabarisha: ´Umar bin Sulaymaan amenihadithia, kutoka kwa ´Abdur-Rahmaan bin Abaan bin ´Uthmaan, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Zayd bin Thaabit, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye amesema:

“Yule ambaye nia yake ni dunia, basi Allaah huliparanganisha jambo lake na huweka ufukara wake baina ya macho yake, na hatochukua kutoka humo isipokuwa kile alichoandikiwa. Na yule ambaye nia yake ni Aakhirah, basi Allaah humkusanyia jambo lake na huweka utajiri wake ndani ya moyo wake, basi hapo itamjilia dunia hali ya kuwa haitaki.”[1]

164 – ´Abbaas bin al-Waliyd bin Shujaa´ an-Narsiy ametukhabarisha: ´Abdullaah bin Yaziyd ametukhabarisha: ar-Rabiy´ bin Subayh ametukhabarisha, kutoka kwa Yaziyd ar-Raqaashiy, kutoka kwa Anas bin Maalik, ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule ambaye nia yake ni kuitafuta Aakhirah, basi Allaah huweka utajiri wake ndani ya moyo wake na akamkusanyia jambo lake, basi hapo itamjilia dunia hali ya kuwa haitaki. Na yule ambaye nia yake ni kuitafuta dunia, basi Allaah huweka ufukara wake baina ya macho yake na huliparanganisha jambo lake na haitomjilia dunia isipokuwa kile alichoandikiwa.”[2]

165 – Muhammad bin Yahyaa ametukhabarisha mfano wa maana hiyo: Daawuud bin al-Muhabbar bin Qahdham ametukhabarisha: Hammaam ametukhabarisha, kutoka kwa Qataadah, kutoka kwa Anas, kutoka kwa Mtume wa Allah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

166 – al-Hulwaaniy ametukhabarisha: Yaziyd bin Haaruun ametukhabarisha: ´Aaswim bin Muhammad ametukhabarisha, kutoka kwa nduguye ´Umar bin Muhammad, kutoka kwa ´Abdullaah bin Diynaar, au Naafiy´, kutoka kwa Ibn ´Umar, ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kufanya hamu yake yote ni jambo moja, basi Allaah atamtosheleza hamu yake kutokana na dunia na Aakhirah yake na atauweka utajiri wake ndani ya moyo wake. Na yule ambaye hamu yake imeparanganyika, basi Allaah hajali ni kwenye bonde gani la ardhi ataangamia.”[3]

167 – Muhammad bin Fudhwayl ametukhabarisha: Muhammad bin Bishr ametukhabarisha: Junayd bin al-´Alaa’ bin Abiy Wahr ametukhabarisha, kutoka kwa Muhammad bin Sa´iyd, kutoka kwa Ismaa´iyl bin ´Ubaydillaah, kutoka kwa Umm-ud-Dardaa’, kutoka kwa Abud-Dardaa’, kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye amesema:

“Jikomboeni kutokana na masimanzi ya dunia kadiri mwezavyo. Kwani yule ambaye dunia ndio hamu yake kubwa, basi Allaah ataparanganisha jambo lake na atauweka ufukara wake baina ya macho yake. Na yule ambaye Aakhirah ndio hamu yake kubwa, basi Allaah atamkusanyikia jambo lake na atauweka utajiri wake ndani ya moyo wake.”[4]

[1] Ibn Maajah (4105). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (3168).

[2] at-Tirmidhiy (2465). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-ul-Jaamiy´” (6510).

[3] al-Haakim (2/443), ambaye amesema kuwa cheni ya wapokezi ni Swahiyh na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[4] Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf-ul-Jaamiy´” (2467).

  • Muhusika: Imaam Abu Bakr Ahmad bin Abiy ´Aaswim ash-Shaybaaniy (a.f.k. 287)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-uz-Zuhd, uk. 40-41
  • Imechapishwa: 07/07/2025