Miongoni mwa adabu zake zilizo thabiti ni kuwa na pupa katika kujifunza na kuendelea nayo katika nyakati zote anazoweza. Asiridhike na kidogo huku anaweza kupata kingi. Asijilazimishe yasiyomwezekana kwa kuogopa kuchoka na kupotea kwa alichopata, jambo ambalo hutofautiana kutegemea watu na hali.

Anapokuja katika kikao cha mwalimu na hakumkuta, asubiri na akae mlangoni mwake. Asikose ratiba yake isipokuwa akiogopa mwalimu kuchukia hilo kwa kujua hali yake kuwa hufundisha katika wakati maalum na hafundishi nje ya wakati huo.

Akimkuta mwalimu amelala au ameshughulika na jambo muhimu, basi asiombe ruhusa ya kuingia. Bali avumilie mpaka aamke, amalize au aondoke. Hata hivyo kuvumilia ndio bora zaidi, kama alivyokuwa akifanya Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) na wengineo.

Inampasa ajilazimishe kufanya jitihada katika kupata elimu wakati wa nafasi, uchangamfu, nguvu za mwili, umakini wa akili na uchache wa mambo yanayomshughulisha kabla ya kuja kwa mambo ya uvivu na kupanda kwa cheo. Kiongozi wa waumini ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Jifunzeni elimu kabla hamjawa mabwana.”[1]

Maana yake ni kwamba fanyeni juhudi kukamilisha uwezo wenu mkiwa bado ni wafuasi kabla ya kuwa viongozi, kwani mkishakuwa viongozi wanaofuatwa basi mtazuiwa kujifunza kwa sababu ya kupanda daraja lenu na wingi wa shughuli zenu. Hii ndiyo maana ya maneno ya Imaam ash-Shaafi´iy (Radhiya Allaahu ´anh):

”Jifunze kabla ya kuwa kiongozi, kwani ukishakuwa kiongozi hakuna njia ya kujifunza.”

[1] Kitaab-ul-´Ilm (9) ya Abu Khaythamah.

  • Muhusika: Imaam Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy (afk. 677)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tibyaan fiy Aadaabi Hamalat-il-Qur-aan, uk. 36
  • Imechapishwa: 26/08/2026