123 – Imesihi kutoka kwa Thaabit, kutoka kwa Anas ambaye amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisoma:

فَلَمَّا تَجَلَّىٰ رَبُّهُ لِلْجَبَلِ جَعَلَهُ دَكًّا وَخَرَّ مُوسَىٰ صَعِقًا

”Mola wako alipojidhihirisha katika jabali akalifanya livurugike kuwa vumbi na Muusa akaanguka hali ya kuzimia.”[1]

Akaweka kidole gumba karibu na ncha ya kidole chake kidogo. Ndipo mlima ukaanguka.”

Humayd akasema kumwambia Thaabit bin al-Bunaaniy: ”Unasema hivo?” Ndipo Thaabit akainua mkono wake, akakipiga kifua cha al-Humayd na kusema: ”Je, nifiche aliyoyasema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Anas? Wewe ni nani, ee Humayd? Wewe ni nani, ee Humayd?”

Hadiyth ni kwa sharti za Muslim.

124 – ´Abdullaah bin ´Amr amesimulia kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

”Hakika nyoyo zote za wanadamu ziko kati ya vidole viwili katika vidole vya Mwingi wa huruma (´Azza wa Jall), kama ulivyo moyo mmoja; anazigeuza vile Anavyotaka.” Kisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Ee Allaah, Mwenye kuzigeuza nyoyo! Ugeuze moyo wangu katika utiifu Wako.”[2]

Ameipokea Muslim.

Hadiyth hii wameipokea Maswahabah kadhaa, akiwemo an-Nawwaas bin Sam´aan, Abu Dharr, Jaabir bin ´Abdillaah, Anas bin Maalik, Nu´aym bin Hammaad, ´Abdullaah bin ´Amr, Umm Salamah, Abu Hurayrah na Swaburah bin Faatik al-Asdiy (Radhiya Allaahu ´anhum).

125 – Ahmad bin Naswr amesema:

”Baada ya kumuuliza Sufyaan bin ´Uyaynah kwa king´ang´anizi nikamsikia anasema nyumbani kwake baada ya ´Ishaa:

”Niache nipumue.” Nikasema: ”Ee Abu Muhammad! Kuna jambo nataka kukuuliza.” Akasema: ”Usiulize.” Nikasema: ”Lazima nikuulize. Vinginevyo nimuulize nani?” Akasema: ”Hebu.” Nikasema: ”Ni vipi kuhusu Hadiyth kutoka kwa ´Ubaadah, kutoka kwa ´Abdullaah, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Je, umepata khabari kwamba Allaah (´Azza wa Jall) ataziweka mbingu kwenye kidole, ardhi kwenye kidole… ”

”Hakika nyoyo za wanadamu ziko kati ya vidole viwili katika vidole vya Mwingi wa huruma (´Azza wa Jall)… ”

”Allaah (´Azza wa Jall) anastaajabu na kucheka.”?

Sufyaan akasema: ”Ni kama zilivyopokelewa. Tunazithibitibisha na kuzisimulia bila kuzifanyia namna.”[3]

Ameipokea Abu Ya´laa al-Farraa’ katika “Ibtwaal-ut-Ta’wiyl” na ad-Daaraqutwniy katika “Kitaab-us-Swifaat”.

126 – Ibn Battwah amesema: Ibn Makhlad ametuhadithia: Muhammad bin al-Muthannaa as-Simsaar ametuhadithia: Nimemsikia Bishr bin al-Haarith akisema:

”Hukumsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

”Hakika nyoyo za wanadamu ziko kati ya vidole viwili katika vidole vya Allaah (´Azza wa Jall).”?

Hawa Jahmiyyah wanazifanyia jeuri.”[4]

[1] 7:143

[2] Muslim (2654), Ahmad (2/168) na an-Nasaa’iy (7739).

[3] Kitaab-us-Swifaat (65) ya ad-Daaraqutwniy.

[4] ash-Shariy´ah, uk. 318, ya al-Aajurriy.

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy (afk. 748)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Arba´iyn fiy Swifaati Rabb-il-´Aalamiyn, uk. 127-132
  • Imechapishwa: 10/06/2024