27. Inatosha kwa muislamu kutamka shahaadah bila ya kulazimiana na masharti yake?

Swali la 27: Kuna dalili gani juu ya uwekwaji Shari´ah ya masharti ya ”Laa ilaaha illa Allaah” katika elimu, unyenyekevu, utakasifu wa nia, mapenzi, kuikubali na yakini? Ni ipi hukumu ya mwenye kusema kwamba inatosha kutamka shahaadah bila ya masharti haya?

Jibu: Imetangulia kubainisha ya kwamba neno la Tawhiyd ni lazima liwe na masharti na kwamba masharti hayo yamejulishwa na dalili za Qur-aan na Sunnah. Amesema  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

“Yeyote atakayesema ”hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah hali ya kuwa mtakasifu moyoni mwake ataingia Peponi”.”

“Yeyote atakayesema ”hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah hali ya kuwa mkweli ndani ya moyo wake… ”.”

“Yeyote atakayesema ”hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na akakufuru na vile vinavyoabudiwa badala ya Allaah… ”.”

Unyenyekevu ni jambo la lazima kwa sababu ni lazima yapatikane matendo. Ni lazima masharti hayo yapelekee katika unyenyekevu. Kadhalika kukubali. Hayo ni masharti yaliyofahamishwa na dalili za Qur-aan na Sunnah; utakasifu wa nia na kutokuwa na shaka, ukweli na yakini, mambo ambayo yanapelekea kukubali na mapenzi. Dalili hizi za Qur-aan na Sunnah zimejulisha ni lazima yapatikane masharti haya. Mwenye kutamka shahaadah kwa mdomo tu bila kushikamana na masharti haya katika utakasifu wa nia, ukweli, mapenzi na unyenyekevu ni mshirikina. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayesema ”hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na akakufuru na vile vinavyoabudiwa badala ya Allaah imeharamika kuporwa mali na kumwagwa damu yake na hesabu yake iko kwa Allaah.

Huyu hakukufuru vile vinavyoabudiwa badala ya Allaah. Hiyo ina maana kwamba hakufanyia kazi masharti haya na hivyo neno lake la Tawhiyd linachenguka kwa vile amelitamka kwa mdomo wake na akalichengua kwa kitendo chake, kwa sababu ”hapana mungu isipokuwa Allaah” maana yake ni hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Akimwabudu mwengine asiyekuwa Allaah amelichengua neno hili. Hukumu ni hiyohiyo pale ataposema ”hapana mungu isipokuwa Allaah” kwa uwongo na si mkweli na ni mnafiki. Allaah amemkufurisha pale aliposema:

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ آمَنَّا بِاللَّـهِ وَبِالْيَوْمِ الْآخِرِ وَمَا هُم بِمُؤْمِنِينَ

“Na miongoni mwa watu wako wasemao: ”Tumemuamini Allaah na Siku ya Mwisho”, hali ya kuwa si wenye kuamini.”[1]

Vielvile amesema (Ta´ala):

إِذَا جَاءَكَ الْمُنَافِقُونَ قَالُوا نَشْهَدُ إِنَّكَ لَرَسُولُ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ إِنَّكَ لَرَسُولُهُ وَاللَّـهُ يَشْهَدُ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَكَاذِبُونَ

”Watakapokujia wanafiki wakisema: “Tunashuhudia kwamba wewe bila shaka ni Mtume wa Allaah.” – na Allaah anajua vyema kuwa hakika wewe ni Mtume Wake na Allaah anashuhudia kuwa hakika wanafiki bila shaka ni waongo.”[2]

Kwa hivyo ikabainika ya kwamba masharti haya yamejulishwa na dalili za Qur-aan na Sunnah na kwamba yakikosekana masharti basi ni lazima mtu atumbukie katika shirki. Mshirikina ni kafiri kwa mujibu wa Qur-aan, Sunnah na maafikiano. Amesema (Ta´ala):

لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ

“Ukifanya shirki bila shaka yataporomoka matendo yako.”[3]

وَمَن يَكْفُرْ بِالْإِيمَانِ فَقَدْ حَبِطَ عَمَلُهُ

”Yeyote atakayekanusha imani, basi yameporomoka matendo yake.”[4]

وَقَدِمْنَا إِلَى مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاء مَّنثُورًا

”Na Tutayaendea yale waliyoyatenda ya matendo yoyote yale na Tutayafanya kuwa ni mavumbi yaliyotawanyika.”[5]

وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Lau wangemshirikisha bila shaka yangeporomoka yale waliyokuwa wakitenda.”[6]

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa, lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[7]

إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ

“Hakika yule atakayemshirikisha Allaah, basi hakika Allaah atamharamishia Pepo na makazi yake yatakuwa ni motoni – na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kuwanusuru.”[8]

Asipolazimiana na masharti haya anatambukia ndani ya shirki. Akiyatamka na asitekeleze haki yake anakuwa pia mshirikina, kwa sababu anakuwa ni mwenye kuipa mgongo dini ya Allaah. Kwa hiyo ikabainika ya kwamba masharti hayo yamefahamishwa na dalili za Qur-aan na kwamba neno hili la Tawhiyd ni lazima yatimiziwe masharti haya. Vinginevyo halina faida yoyote.

[1] 02:08

[2] 63:01-02

[3] 39:65

[4] 5:5

[5] 25:23

[6] 06:88

[7] 4:48

[8] 05:72

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah wa Ajwibah fiy-Iymaan wal-Kufr, uk. 59-62
  • Imechapishwa: 09/01/2026