Kwa hiyo ndugu zangu jitahidini kusoma Qur-aan tukufu na khaswa katika mwezi huu ambao imeteremshwa ndani yake. Hakika kuisoma kwa wingi kuna sifa ya kipekee. Jibriyl alikuwa akimdhihirishia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Qur-aan katika Ramadhaan kila mwaka mara moja. Ilipokuwa ule mwaka ambao alikufa ndani yake akamdhihirishia mara mbili kwa ajili ya kuisimika na kuithibitisha.

as-Salaf as-Swaalih (Raadhiya Allaahu ´anhum) walikuwa wakikithirisha kuisoma Qur-aan katika Ramadhaan ndani ya swalah na kwenginepo. az-Zuhriy (Rahimahu Allaah) wakati inapoingia Ramadhaan alikuwa akisema:

“Hakuna kazi nyingine isipokuwa kusoma Qur-aan na kulisha chakula.”

Maalik (Rahimahu Allaah) wakati inapoingia Ramadhaan alikuwa anaacha kusoma Hadiyth, vikao vya elimu na akielekea kusoma Qur-aan ndani ya msahafu.”

Qataadah (Rahimahu Allaah) alikuwa daima akisomaa Qur-aan nzima kila baada ya wiki moja. Ramadhaan akiisoma yote kila baada ya nyusiku tatu. Lile kumi la mwisho la Ramadhaan akisoma Qur-aan yote ndani ya nyusiku mbili.

Ibraahiym an-Nakha´iy (Rahimahu Allaah) alikuwa akisoma Qur-aan yote katika Ramadhaan kila baada ya nyusiku tatu. Kumi la mwisho akiisoma yote kila baada ya nyusiku mbili.

al-Aswad (Rahimahu Allaah) alikuwa akiisoma Qur-aan yote ndani ya nyusiku mbili akifanya hivo mwezi mzima.

Hivyo basi waigilizeni wabora hawa na fuateni mfumo wao mtakuwa pamoja na wema na watwaharifu. Tumieni fursa ya saa za nyusiku na mchana kwa yale yanayokukurubisheni kwa Mwenye nguvu zisizoshindika na Mwingi wa kusamehe. Hakika umri unakimbia kwa haraka na nyakati zinaisha zote kama kwamba ni saa moja tu ya mchana.

Ee Allaah! Turuzuku kukisoma Kitabu Chako kwa njia inayokuridhisha na tuongoze kwayo njia za salama na utuondoshe kupitia yenyewe kutoka katika viza na kutuingiza katika nuru na uifanye kuwa ni hoja yetu na si hoja dhidi yetu, ee Mola wa walimwengu.

Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 37-38
  • Imechapishwa: 07/04/2020