Swali: Kuna mwanamke amepata hedhi katika mwezi wa Ramadhaan akaendelea kufunga. Ni ipi hukumu?

Jibu: Mwanamke akipata hedhi basi analazimika kuacha kuswali na kufunga. Bali ni haramu kwake kuswali na kufunga kwa maafikiano. Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Sijaona walio na akili punguani na dini pungufu wanaomghalibu mwanaume mwenye busara kama nyinyi [wanawake].” Tukasema: “Ni upi upungufu wa akili na dini yetu, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Je, ushahidi wa mwanamke mmoja si ni sawa na nusu ya ushahidi mwanamme mmoja?” Tukajibu: “Ndio.” Akasema: “Huyo ndio upungufu wa akili zao.” Akasema tena: “Si wanapokuwa na hedhi si haswali na wala hafungi?”Tukajibu: “Ndio.” Akasema: “Hayo ni katika upungufu wa dini yake.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia Faatwimah bint Abiy Hubaysh:

“Inapokuja hedhi yako basi wacha kuswali. Inapoondoka basi jisafishe damu yako kisha uswali.”[2]

Wakati mwanamke mwenye hedhi anapotwahirika, basi analazimika kulipa siku hiyo ikiwa ni ya Ramadhaan. Hata hivyo haikuwekwa katika Shari´ah kulipa swalah. Mu´aadhah amesema:

“Nilimuuliza ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ni kwa nini mwenye hedhi analipa swawm na halipi swalah. Akasema: “Je, wewe ni Haruuriyyah?” Akasema: “Mimi sio Haruuriyyah. Nauliza tu.” Ndipo akasema: “Tulikuwa tukipatwa na kitu hicho wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tunaamrishwa kulipa swawm na wala hatuamrishwi kulipa swalah.”[3]

Kutokana na yaliyotangulia mwanamke huyo amekosea kwa kufunga baadhi ya siku za Ramadhaan ilihali yuko na hedhi. Ni lazima kwake kutubu kwa Allaah kutokana na kitendo hicho na pia analazimika kulipa masiku hayo, kwa sababu masiku yake yaliyotangulia hayazingatiwi ki-Shari´ah.

Kwa mnasaba wa jambo hili ni vizuri kuwazindua dada zetu wa Kiislamu ya kwamba Mwekaji Shari´ah ameifungamanishia hedhi ya mwanamke hukumu ambazo analazimika kujifunza nazo na kuzielewa. Miongoni mwanzo ni kwamba hedhi ni alama ya kubaleghe kwake, ni haramu kwake kujamiwa, kuswali, kufunga, kubaki msikitini na kutufu Nyumba wakati yuko na hedhi. Twahara yake haisihi muda wa kuwa yuko na hedhi na kwamba analazimika kuoga wakati inapokatika. Ni lazima kwa mwanamke wa Kiislamu kuzitambua hukumu hizo na kujifunza nazo kwa mujibu wa dalili zake ili aweze kumwabudu Allaah kwa umaizi. Allaah atuwafikishe sote kuielewa dini Yake na kutendea kazi Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] al-Bukhaariy (304).

[2] al-Bukhaariy (306).

[3] al-Bukhaariy (321) na Muslim (335).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min Fataawaas-Swiyaam, uk. 27-29
  • Imechapishwa: 28/03/2022