26. Matahadharisho ya usomaji Qur-aan kwa lengo la umaarufu na kutaka kusikika

107 – Abul-Hasan ´Aliy bin Ahmad bin ´Umar al-Muqriy’ ametukhabarisha: Muhammad bin al-´Abbaas bin al-Fadhwl ametuhadithia huko Mosul: Muhammad bin Ahmad bin Abiyl-Muthannaa ametuhadithia: Ja´far bin ´Awn na ´Abdul-Wahhaab – yaani Ibn ´Atwaa’ – wametuhadithia: ´Abdul-Malik bin ´Abdil-´Aziyz bin Jurayj ametukhabarisha: Yuunus bin Yuusuf amenikhabarisha, kutoka kwa Sulaymaan bin Yasaar ambaye amesema:

”Watu walitawanyika kutoka kwa Abu Hurayrah ambapo Naatil kutokea Shaam akamwambia: ”Ee mzee! Tuhadithie jambo ulilolisikia kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Akasema: ”Ndio.”  Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema: “Watu wa mwanzo wataohukumiwa siku ya Qiyaamah ni ambaye alikufa shahidi. Ataletwa mbele ambapo atatambulishwa neema Zake azitambue. Kusemwe: ”Ulizifanyisha nini?” Atasema: ”Nilipambana kwa ajili Yako mpaka nikafa shahidi.” Aseme: ”Mwongo. Hakika mambo yalivyo ni kwamba ulipigana ili uambiwe kuwa ni shujaa, na kumeshasemwa.” Kisha kuamrishwe aburuzwe kwa uso wake mpaka atupwe ndani ya Moto. Mwingine ni mtu ambaye alijifunza elimu, akaifunza na akajifunza Qur-aaan. Ataletwa mbele ambapo atatambulishwa neema Zake azitambue. Kusemwe: ”Ulizifanyisha nini?” Atasema: ”Nilijifunza elimu, nikaifunza na nikajifunza Qur-aan kwa ajili Yako.”  Aseme: ”Mwongo. Hakika mambo yalivyo ni kwamba ulitaka uambiwe kuwa ni mwanachuoni na msomaji, na kumeshasemwa.” Kisha kuamrishwe aburuzwe kwa uso wake mpaka atupwe ndani ya Moto. Mtu mwingine alitajirishwa na kupewa aina mbalimbali ya mali. Ataletwa mbele ambapo atatambulishwa neema Zake azitambue. Kusemwe: ”Ulizifanyisha nini?” Atasema: ”Sikuacha njia yoyote ambayo Unapenda kutolewe kwa ajili Yako, isipokuwa nilitoa kwa ajili Yako.” Aseme: ”Mwongo. Hakika mambo yalivyo ni kwamba ulichotaka ni kusemwe kwamba wewe ni mkarimu, na kumeshasemwa.” Kisha kuamrishwe aburuzwe kwa uso wake mpaka atupwe ndani ya Moto.”[1]

108 – Abul-Husayn ´Aliy bin Muhammad bin ´Abdillaah bin Bishraan al-Mu-addil ametukhabarisha: Ismaa´iyl bin Muhammad bin Ismaa´iyl as-Swaffaar ametuzindua: Muhammad bin ´Ubaydillaah bin al-Munaadiy ametuhadithia: Abu Badr ametukhabarisha: ´Amr bin Qays ametukhabarisha, kutoka kwa al-Hasan, aliyesema:

”Hakika wamejifunza Qur-aan hii waja na watoto kimakosa na pasi na kujua tafsiri yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ لِّيَدَّبَّرُوا آيَاتِهِ وَلِيَتَذَكَّرَ أُوْلُوا الْأَلْبَابِ

“Kitabu Tumekiteremsha kwako chenye baraka ili wapate kuzingatia kwa makini Aayah zake na ili wapate kukumbuka wale wenye akili.”[2]

Ni vipi zinazingatiwa Aayah zake? Ni kwa kuzifanyia kazi. Hakika watu wenye haki zaidi na Qur-aan hii ni wale wanaoifuata licha ya kwamba hawaisomi. Mmoja wao anaweza kusema ´Hebu njoo nikusomee`. Ni lini wasomaji walikuwa wakifanya hivo? Si wasomaji, wapole wala wenye hekima. Allaah asifanye watu kama hawa wakawa wengi kati ya watu!”

109 – Muhammad bin al-Husayn al-Qattwaan ametukhabarisha: Da´laj bin Ahmad ametuzindua: Muhammad bin ´Aliy bin Zayd as-Swaa-igh ametukhabarisha kwamba Sa´iyd bin Mansuur amewahadithia: Hudayth – yaani Ibn Mu´aawiyah – ametuhadithia, kutoka kwa Abu Ishaaq: ´Umar bin al-Khattwaab amesema:

”Asikughurini anayeisoma Qur-aan. Hakika mambo yalivyo ni maneno tu tunayoyatamka.  Badala yake mtazameni yule anayeifanyia kazi.”

[1] Swahiyh. Ameipokea Muslim (1905) kupitia njia nyingi kutoka kwa Ibn Jurayj.

[2] 38:29

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr Ahmad bin ´Aliy al-Khatwiyb al-Baghdaadiy (afk. 463)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Iqtidhwaa’-ul-´Ilm al-´Amal, uk. 69-71
  • Imechapishwa: 15/05/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy