Qaadhwiy na Imaam Abu Ya’laa amesema:

“Haijuzu kuzirudisha nyuma Hadiyth hizi wala kujishughulisha kwa kuzipindisha maana. Wajibu ni kuzielewa kwa maana yake ya dhahiri na kwamba hizi ni sifa za Allaah ambazo hazifanani na sifa za viumbe walioelezewa kwa mfano wake. Kinachothibitisha ubatilifu wa kupindisha maana ni kwamba Maswahabah na waliowafuata miongoni mwa wanfunzi wao walizichukulia kwa maana zake za dhahiri na hawakujihusisha kuzipindisha maana wala kuziepusha na dhahiri yake. Ikiwa inafaa kupindisha maana, basi wao wangelitangulia kufanya hivyo kwa madai ya kuondoa ufananishaji.”[1]

Kwa maana kujengea msingi wa wale wanaosema kuwa dhahiri yake ni kufananisha.

Amesema tena katika mnasaba wa Hadiyth ya kijakazi:

“Fahamu kwamba mazungumzo juu ya Hadiyth hii yako katika sehemu mbili:

1 – Inajuzu kuuliza juu Yake (Subhaanah) mahali alipo na kwamba inajuzu kujibu kwamba Yuko juu ya mbingu.

2 – Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwache huru. Kwani hakika ni muumini.”

Swali la kwanza liko wazi. Swali linapelekea kuwa inafaa na kwamba inafaa pia kujibu kwamba yuko juu ya mbingu. Kwani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia kijakazi:

“Allaah yuko wapi?”

Kama isingelikuwa inafaa basi asingeuliza hivo. Alijibu kuwa yuko juu ya mbingu na kwamba akamkubalia jawabu lake. Kama isingelikuwa inafaa kujibu kuwa Yeye (Subhaanah) yuko juu ya mbingu basi asingemkubalia… Ahmad amezungumzia mada hiyo kwa kina na akasema katika ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah”:

”Isitoshe Allaah ametueleza ya kwamba Yuko juu ya mbingu. Amesema:

أَأَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يَخْسِفَ بِكُمُ الْأَرْضَ

“Je, mnadhani mko katika amani na aliyeko juu mbinguni kwamba hatokudidimizeni ardhini?”[2]

إِلَيْهِ يَصْعَدُ الْكَلِمُ الطَّيِّبُ وَالْعَمَلُ الصَّالِحُ يَرْفَعُهُ

“Kwake pekee linapanda neno zuri na kitendo chema anakiinua juu.”[3]

يَا عِيسَى إِنِّي مُتَوَفِّيكَ وَرَافِعُكَ إِلَيَّ

“Ee ‘Iysaa! Hakika Mimi ni Mwenye kukuchukua na Mwenye kukupandisha Kwangu.”[4]

Sambamba na hilo Yuko juu ya ´Arshi na ujuzi Wake umekizunguka kila kitu kilicho chini ya ´Arshi.”[5][6]

[1] Ibtwaal-ut-Ta’wiyl (1/71).

[2] 67:16

[3] 35:10

[4] 3:55

[5] ar-Radd ´alAAl-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah, uk. 142-150.

[6] Ibtwaal-ut-Ta’wiyl (1/232).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad bin ´Abdil-Haadiy al-Maqdisiy (afk. 744)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Kalaam ´alaa Mas-alat-il-Istiwaa’ ´alaal-´Arsh, uk. 85-86
  • Imechapishwa: 29/12/2025