Swali 25: Wapo watu ambao ni washabiki wa madhehebu au mwanachuoni wakati wengine wanawapuuza na kupuuzia nasaha za wanazuoni na maimamu. Unasemaje juu ya hilo?

Jibu: Ni kweli. Watu aina mbili hawa ni wenye kutofautiana.

Kundi moja ni lenye kufuata kipofu kwa kiasi cha kwamba wanafuata kichwa mchunga maoni ya watu hata kama yatakuwa ni yenye kwenda kinyume na dalili. Hili ndio jambo lenye kukemewa na linaweza kupelekea katika kufuru[1].

Kundi lingine linatupilia mbali maneno ya wanazuoni na hawanufaiki nayo hata kama yatakuwa ni yenye kuafikiana na Qur-aan na Sunnah.

Kundi la kwanza ni lenye kupetuka mipaka na la pili ni lenye kuzembea.

Kuna kheri katika maneno ya wanazuoni na khaswa maneno ya Salaf; uelewa wa Maswahabah na wanafunzi wa Maswahabah,  maimamu wanne na wanazuoni ambao uelewa wao umethibitishwa na ummah. Inatakikana kufaidika na kunufaika na maoni yao. Lakini si kwamba yatachukuliwa mia kwa mia. Pale tunapojua kuwa kuna maoni yenye kwenda kinyume na dalili, basi ni wajibu kwetu kufuata dalili. Ama tunapojua kuwa haiendani kinyume na dalili katika Qur-aan na Sunnah, ni sawa kuifuata. Huu sio ushabiki. Ni njia moja wapo ya kunufaika na uelewa wa Salaf na kuielewa Qur-aan na Sunnah. Haya ndio maoni ya haki na yaliyo kati na kati. Tunakubali maneno ya wanazuoni pale ambapo yanaafikiana na dalili katika Qur-aan na Sunnah na kuacha yale yenye kutofautiana na dalili. Pamoja na hivyo tunawapa udhuru wanazuoni kwa makosa yao, tunaitambua nafasi yao na wala hatuwatii upungufu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakimu akihukumu na akajitahidi na kupatia, anapata ujira mara mbili. Na akihukumu na kujitahidi na kukosea, anapata ujira mara moja.”[2]

Kosa ni lenye kusamehewa ikiwa linatokamana na mtu ambaye anastahiki kufanya Ijtiaad. Mjinga na mtu ambaye ndio sasa ameanza kutafuta elimu hana haki yoyote ya kufanya Ijtihaad. Haifai kwao kufanya Ijtihaad. Wanapata dhambi kwa kufanya Ijtihaad ni mamoja wakipatia au wakikosea. Kwa sababu wamefanya kitu wasichokistahiki.

[1] Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Yule anayefanya ushabiki kwa mtu maalum, mbali na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama kufanya ushabiki kwa Maalik, Ahmad, ash-Shaafi´iy au Abu Haniyfah na akaona kuwa maoni yake ndio ya sawa ambayo unatakiwa kufuatwa pasi na Imaam mwingine yeyote ambaye anaenda kinyume naye, mtu huyo ni mjinga na mpotevu. Bali anaweza kuwa kafiri. Yule mwenye kuamini kuwa ni wajibu kumfuata mmoja kati ya maimamu hawa wanne pasi na mwingine yeyote ni wajibu atubu. Akitubia ni sawa na vinginevyo auliwe.” (Madjmuu´-ul-Fataawaa (22/248-249))

[2] al-Bukhaariy (6919) na Muslim (1716).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 74-75
  • Imechapishwa: 31/05/2023