6 – Kichenguzi cha sita cha wudhuu´: Kula nyama ya ngamia. Kuhusu wudhuu´ kwa anayekula nyama ya ngamia kuna mitazamo miwili ya wanazuoni:

1 – Maoni ya kikosi kikubwa cha wanazuoni ambao wanaona kuwa halazimiki kutawadha kwa kula nyama hiyo.

2 – Ni kuwa wudhuu´ ni wa lazima kwa anayekula nyama ya ngamia. Ni mamoja nyama hiyo ni mbichi au iliyopikwa. Kuhusu maziwa, supu yake na chakula kilichopikwa pamoja na nyama hiyo, basi matumizi yake haya hayachengui wudhuu´. Dalili ya kwamba anayekula nyama ya ngamia anapaswa kutawadha ni Hadiyth ya Jaabir bin Samurah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameleeza kwamba:

“Mtu mmoja alimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): ”Je, nitawadhe baada ya kula nyama ya kondoo au mbuzi?” Akajibu: ”Ukitaka tawadha, ukitaka usitawadhe.” Akauliza: ”Je, nitawadhe baada ya kula nyama ya ngamia?” Akajibu: ”Ndio, tawadha baada ya kula nyama ya ngamia.” Akauliza: ”Je, niswali katika mazizi ya kondoo na mbuzi?” Akajibu: ”Ndiyo.” Akauliza: ”Je, niswali katika maeneo ya mapumziko ya ngamia?” Akajibu: ”Hapana.”

Ameipokea Muslim (360).

Hadiyth ya al-Barraa’ bin ´Aazib (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameleeza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa kuhusu kutawadha baada ya kula nyama ya ngamia?” Akajibu: ”Tawadheni baada yake.” Akaulizwa kuhusu nyama ya kondoo na mbuzi?” Akajibu: ”Msitawadhe baada yake.” Akaulizwa kuhusu swalah katika mapumziko ya ngamia?” Akajibu: ”Msiswali maeneo ya ngamia, kwani ni sehemu za mashaytwaan.” Akaulizwa kuhusu swalah katika mazizi ya kondoo na mbuzi?” Akajibu: ”Swalini humo, kwani kuna baraka.”

Ameipokea Abu Daawuud (184) na wengine na cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.

Msingi wa amri ni kwamba ni wajibu. Neno “wudhuu´” linamaanisha wudhuu´ wa Kishari´ah. Hivyo amri isifasiriwe kwamba inapendeza wala isifasiriwe kuwa ni wudhuu´ wa kilugha ambao ni kuosha mikono na kusukutua mdomo, kwa sababu hakuna kilichogeuza kutoka kwenye msingi. Tazama ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (118).

an-Nawawiy ametaja katika ”Sharh Swahiyh Muslim” (4/49) kuhusu makinzano ya wanazuoni kuhusu kutawadha baada ya kula nyama ya ngamia akasema: “Ahmad bin Hanbal na Ishaaq bin Raahuuyah wamesema kuhusu hili – bi maana kutawadha baada ya kula nyama ya ngamia – kuna Hadiyth mbili: ”Hadiyth ya Jaabir na ya al-Barraa’.” Madhehebu haya yana dalili yenye nguvu zaidi, japokuwa wanazuoni wengi wanaonelea kinyume na hivo.” Tazama ”Majmuu´-ul-Fataawaa” (10/156–158) ya Shaykh Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) na ”Fataawaa al-Lajnah ad-Daa’imah” (5/273–277).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 26-27
  • Imechapishwa: 26/05/2026