25. Kuamini kuonekana kwa Allaah Aakhirah

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Inatakiwa kuamini kuonekana kwa Allaah siku ya Qiyaamah. Kumepokelewa Hadiyth nyingi Swahiyh kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusiana na suala hili. Inatakiwa pia kuamini kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola Wake. Imepokelewa Swahiyh kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Qataadah amepokea hilo kutoka kwa ´Ikrimah, kutoka kwa Ibn ´Abbaas.

al-Hakam bin Abaan amepokea hilo kutoka kwa ´Ikrimah, kutoka kwa Ibn ´Abbaas.

´Aliy bin Zayd amepokea hilo kutoka kwa Yuusuf bin Mahraan, kutoka kwa Ibn ´Abbaas.

Tunaiamini Hadiyth hii kama ilivyo kama jinsi ilivyopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni uzushi kuzungumzia juu ya hilo. Tunaliamini kama lilivyo kama jinsi ilivyofikishwa na hatujadili na yeyote juu ya suala hili.”

MAELEZO

 Kuna maoni tofauti juu ya suala hili. Je, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) alimuona Mola wake wakati wa Safari ya mbinguni au hapana? Baadhi ya watu wameshikamana na maneno ya Ibn ´Abbaas na Ahmad na kufahamu ya kwamba wote wawili wanasema kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola wake kwa macho Yake. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema kuwa maneno ya Ahmad na ya Ibn ´Abbaas yametajwa kwa kuachiwa na kwa kufungamanishwa. Ibn ´Abbaas amesema pasi na kufungamanisha kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola wake na kwa kufungamanisha kwamba alimuona kwa moyo wake. Vivyo hivyo Ahmad. Maneno ya Ibn Taymiyyah ni kweli. Hakuna dalili katika Qur-aan wala Sunnah ya kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona kikweli Mola wake. Maneno ya Ibn ´Abbaas ni ya kwake mwenyewe na pia yamefungamanishwa. Maandiko yaliyofungamanishwa ndio sahihi zaidi. Katika “as-Swahiyh”[1] ya Muslim kuna ambavyo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola wake kwa moyo wake mara mbili.  Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

مَا كَذَبَ الْفُؤَادُ مَا رَأَىٰ

“Moyo haukukadhibisha yale aliyoyaona.”[2]

وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَىٰ

“Hakika amemuona katika uteremko mwingine.”[3]

Bi maana mara mbili.

Masruuq ameeleza kuwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Ambaye atakueleza mambo matatu basi amemsemea Allaah uongo mkubwa… Mwenye kusema kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola wake amemsemea Allaah uongo mkubwa.” Masruuq akasema: “Ee mama wa waumini! Nipe muda na usinifanyie haraka; Allaah si amesema:

مَا كَذَبَ الْفُؤَادُ مَا رَأَىٰ

“Moyo haukukadhibisha yale aliyoyaona.”[4]

وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَىٰ

“Hakika amemuona katika uteremko mwingine.”?

Akasema: “Mimi nilikuwa mtu wa kwanza katika Ummah huu kumuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya hili na akasema: “Ilikuwa Jibriyl. Sikumuona katika umbile lake la asili isipokuwa mara mbili hizi. Nilimuona akishuka kutoka mbinguni. Umbo lake kubwa lilifunika kila kitu baina ya mbingu na ardhi.”

Aayah inahusiana na Muhammad kumuona Jibriyl (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam).

Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa kama alimuona Mola wake ambapo akajibu kwa kusema:

“Ni nuru. Vipi nitamuona?”

Bi maana ni jambo liko mbali kabisa.

Isitoshe milolongo miwili iliyotajwa kwenda kwa Ibn ´Abbaas ina udhaifu. Katika upokezi mmoja kuna al-Hakam bin Abaan ambaye ni mwaminifu lakini husimulia makosa[5]. Katika upokezi mwingine kuna ´Aliy bin Zayd bin Jud´aan ambaye ni mdhaifu[6]. Kwenye upokezi huo mna Yuusuf bin Mahraan ambaye hajulikani na ´Aliy bin Zayd bin Jud´aan peke yake ndiye amepokea kutoka kwake. Mapokezi haya mawili ni maneno ya Ibn ´Abbaas. Ni maneno yepi yenye kutangulizwa yakioanishwa maneno ya Ibn ´Abbaas na ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam)? Hapa ni pale tukichukulia kuwa Ibn ´Abbaas alisema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam) alimuona Mola wake kwa macho yake. Vinginevyo ni kwamba upokezi huu katika tukio la uhalisia unafungamanishwa na upokezi uliyothibiti wenye kusema kuwa (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam) alimuona Mola wake kwa moyo. Ibn ´Abbaas mwenyewe ameyafungamanisha maneno yake ambayo hayakufungana. Ibn Taymiyyah amesema kuwa Imaam Ahmad amefanya hali kadhalika. Sahihi ni kwamba mapokezi haya yanatakiwa kufahamika kwa njia ya kufungamanishwa.

[1] Muslim (176).

[2] 53:11

[3] 53:13

[4] 53:11

[5] Ibn Hajar amesema:

”Mwaminifu na mfanya ´ibaadah ambaye husimulia makosa.” (at-Taqriyb)

[6] Ibn Hajar amesema:

”Mdhaifu.” (at-Taqriyb)