Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisoma Suurah nyingine baada ya al-Faatihah. Wakati fulani alikuwa akiisoma kwa kuirefusha na wakati mwingine alikuwa akisoma kwa kuifupisha kutokana na sababu ya safari, kukohoa, maradhi au kulia kwa mtoto. Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Siku moja aliswali (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Fajr fupi.”[1]

Katika upokezi mwingine kumesimuliwa namna ambavyo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswali Fajr kwa Suurah mbili fupi katika Qur-aan. Kukasemwa: “Ee Mtume wa Allaah! Kwa nini umefupisha?” Akajibu:

“Nimesikia kilio cha mtoto, nikafiri kuwa mama yake anaswali pamoja na sisi ambapo nikataka mama yake amwangalie.”[2]

Amesema vilevile:

“Hakika mimi huingia ndani ya swalah hali ya kuwa nataka kuirefusha. Pindi ninaposikia kilio cha mtoto huifupisha swalah yangu kwa vile naelewa yale machungu ya mama yake kwa kile kilio chake.”[3]

Mara nyingi alikuwa akiianza Suurah mwanzo na kuikamilisha[4].

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ipeni kila Suurah sehemu yake katika Rukuu´ na Sujuud.”[5]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Kila Suurah ina Rak´ah.”[6]

Wakati mwingine alikuwa anaweza kuigawa Suurah mara mbili katika Rak´ah mbili[7], wakati mwingine akiisoma tena katika hiyo Rak´ah ya pili na wakati mwingine alikuwa anaweza kukusanya Suurah mbili au zaidi baada ya al-Faatihah katika Rak´ah hiyo hiyo moja.

Alikuwepo mwanaume mmoja kutoka katika Answaar akiongoza swalah katika msikiti wa Qubaa´. Alikuwa siku zote akiwasomea Suurah moja. Kila wakati alikuwa akisoma:

قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ

“Sema: “Yeye ni Allaah, Mmoja pekee.”[8]

halafu anaanza na Suurah nyingine tena. Alikuwa akifanya hivo katika kila Rak´ah. Wenzake wakamwambia: “Wewe siku zote huanza kwa Suurah hii kisha hutosheki nayo mpaka unasoma nyingine.” Ima uisome au uachane nayo na badala yake usome nyingine.” Akasema: “Mimi sintoiacha. Mkipenda niendelee kufanya hivo na kuwaswalisha nitafanya na kama hampendi nitawaacheni.” Walikuwa wanamuona yeye ndiye mbora wao na hawakupenda mwingine awaongoze. Pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowajia wakamueleza yaliyopitika. Akasema: “Ee fulani! Ni kipi kinachokuzuia kufanya yale wanayokueleza wenzako? Kipi kinachokufanya wewe siku zote kusoma Suurah hii katika kila Rak´ah?” Akasema: “Mimi naipenda.” Ndipo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Kuipenda kwako kutakuingiza Peponi.”[9]

[1] Hadiyth hii, na nyenginezo mfano wake, kuna dalili juu ya kujuzu kuwaingiza watoto misikitini. Kuhusu Hadiyth inayojulikana inayosema ”Watengeni watoto wenu mbali na misikiti… ”, ni dhaifu na sio hoja kwa maafikiano. Miongoni mwa walioidhoofisha ni Ibn-ul-Jawziy, al-Mundhiriy, al-Haythamiy, Haafidhw Ibn Hajar al-´Asqalaaniy na al-Buuswayriy. ´Abdul-Haqq al-Ishbiyliy amesema:

”Haina msingi.”

[2] Ahmad kwa mlolongo wa wapokezi mzuri. Hadiyth nyingine imepokelewa na Ibn Abiy Daawuud katika ”al-Maswaahif” (2/14/4).

[3] al-Bukhaariy na Muslim.

[4] Kuna Hadiyth nyingi zinazothibitisha hili, kama itakavyokuja huko mbele kidogo kidogo.

[5] Ibn Abiy Shaybah (1/100/1), Ahmad na ´Abdul-Ghaniy al-Maqdisiy katika ”as-Sunan” kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[6] Ibn Naswr na at-Twahaawiy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh. Naonelea kuwa maana ya Hadiyth ni Suurah nzima inatakiwa isomwe katika kila Rak´ah ili kila Rak´ah iwe na hadhi yake kamili kwa hiyo Suurah. Hata hivyo amri ni kwa ajili ya mapendekezo na sio lazima, kama itavyotajwa baadaye.

[7] Ahmad na Abu Ya´laa kupitia njia mbili.

[8] 112:01

[9] al-Bukhaariy kwa mlolongo wa wapokezi pungufu na at-Tirmidhiy kwa kuungana. Ni Swahiyh kwa mujibu wa at-Tirmidhiy.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 89-91
  • Imechapishwa: 04/02/2017