Swali 24: Ni ipi hukumu ya salamu baada ya Sunnah[1]?

Jibu: Ni jambo limewekwa katika Shari´ah kwa wenye kukutana katika safu mmoja akamsalimia mwengine na wakapeana mikono. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna waislamu wawili wanaokutana ambapo wakapeana mikono isipokuwa Allaah huwasamehe kabla hawajaachana.”[2]

Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wanapokutana basi wanapeana mikono na wanapofika kutoka safarini basi wanakumbatiana.”

Vilevile imethibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake hamtoingia Peponi mpaka muamini na wala hamtoamini mpaka mpendane. Je, nisikujulisheni kitu ambacho mkikifanya mtapendana; sambazeni salamu kati yenu.”[3]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Pia aliulizwa ni Uislamu upi bora zaidi ambapo akajibu kwa kusema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kulisha chakula na kumtolea salamu unayemjua na usiyemjua.”[4]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Isipokuwa ambaye umekutana naye unajua kuwa ni kafiri. Katika hali hiyo usianze kumtolea salamu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msianze kuwatolea salamu mayahudi wala manaswara.”[5]

Hadiyth ameipokea Muslim.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/411-412).

[2] at-Tirmidhiy (2651) na Abu Daawuud (4536).

[3] Muslim (81), at-Tirmidhiy (2434) na Ahmad (1355).

[4] al-Bukhaariy (11, 27) na Muslim (56).

[5] Muslim (4030) na at-Tirmidhiy (2624).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 65-66
  • Imechapishwa: 29/11/2021