Aingie kwa mwalimu wake akiwa ametimia sifa kamili, akiwa na sifa tulizozitaja kwa mwalimu, akiwa na twahara, ametumia Siwaak na moyo wake uko huru kutokana na mambo yanayomshughulisha. Asiingie bila kuomba ruhusa ikiwa mwalimu yuko katika mahali panapohitaji ruhusa. Awasalimie waliopo anapoingia na amtenge yeye kwa salamu maalum.

Amsalimie yeye na wao anapoondoka, kama ilivyokuja katika Hadiyth:

”Mmoja wenu anapofika katika kikao basi asalimie. Anapotaka kuketi chini, afanye hivo. Anapotaka kusimama na kuondoka asalimie. Kwani  ya kwanza haina haki zaidi kuliko ya pili.”[1]

Asivuke juu ya shingo za watu. Bali akae pale anapofikia kikao, isipokuwa mwalimu amruhusu kusogea mbele au akajua kutokana na hali yao kuwa wanapendelea hivo. Wala asimsimamishe yeyote kutoka mahali pake. Ikiwa mwingine atampa nafasi, basi asiikubali kwa kumuigiliza Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa), isipokuwa ikiwa katika kutangulia kwake kuna maslahi kwa wahudhuriaji au mwalimu amemwamuru hivyo. Aidha asikae katikati ya duara la kikao isipokuwa kwa dharurah. Asikae kati ya watu wawili bila idhini yao. Ikiwa watampa nafasi akae na asijitanue.

[1] Abu Daawuud (5207) na at-Tirmidhiy (2706), ambaye amesema kuwa Hadiyth ni nzuri. Yenye nguvu zaidi kuliko nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-ul-Kalim at-Twayyib” (160).

  • Muhusika: Imaam Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy (afk. 677)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tibyaan fiy Aadaabi Hamalat-il-Qur-aan, uk. 34-35
  • Imechapishwa: 26/08/2026