Ee mwanamke wa Kiislamu! Hakika wewe ni mwenye kuaminiwa Kishari´ah juu ya kile anachokiumba Allaah kwenye mfuko wa uzazi wako katika mimba. Kwa hivyo usikifiche. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَلَا يَحِلُّ لَهُنَّ أَن يَكْتُمْنَ مَا خَلَقَ اللَّـهُ فِي أَرْحَامِهِنَّ إِن كُنَّ يُؤْمِنَّ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ

“Wala si halali kwao kuficha aliyoumba Allaah katika matumbo yao ikiwa wao ni wenye kumwamini Allaah na siku ya Mwisho.”[1]

Usifanye hila za kuitoa mimba hiyo na kujikwamua nayo kwa njia yoyote. Hakika Allaah (Subhaanah) amekupa ruhusa ya kula katika Ramadhaan ikiwa swawm inakutia uzito katika hali ya ufungaji na ikiwa swawm inaidhuru mimba yako.

Yale yaliyoenea hii leo katika operesheni za kutoa mimba ni jambo la haramu. Ikiwa kipomoko tayari kimeshapuliziwa roho na hivyo kikafariki kwa sababu ya uporomoshaji mimba, basi huko kunazingatiwa ni kuiua nafsi ambayo Allaah ameharamisha kuiua pasi na haki na hivyo kitendo hicho kitapelekea katika hukumu za uhusikaji wa tendo la jinai kwa njia ya ulazima wa kutoa diyaa kwa mujibu wa upambanuzi wa viwango vyake na kwa njia ya ulazima wa kutoa kafara kwa mtazamo wa baadhi ya maimamu. Kafara yenyewe ni kuacha mtumwa huru ambaye ni muumini. Asipoweza afunge miezi miwili mfululizo. Baadhi ya wanachuoni wameita kitendo hichi kuwa ni uuaji mdogo. Shaykh Muhammad bin Ibraahiym (Rahimahu Allaah) amesema katika “Majmuu´-ul-Fataawaa”:

“Haijuzu kufanya majaribio ya kuporomosha mimba muda wa kuwa hakujathibiti kufa kwake. Kukithibiti kufa kwake basi itafaa.”[2]

Kupitia mathibitisho ya kikao cha baraza la Kibaar-ul-´Ulamaa’, nambari. 140 tarehe 20/06/1407 wamesema yafuatayo:

1 – Haijuzu kutoa mimba katika hatua zake zote isipokuwa kwa jambo linalohalalisha linalokubalika Kishari´ah na katika mipaka midogo sana.

2 – Ikiwa mimba iko katika awamu yake ya kwanza, yaani ndani ya muda wa siku arubaini, na wakati huohuo ikawa katika kule kuiporomosha kuna manufaa ya Kishari´ah au kuzuia madhara basi itafaa kuiporomosha. Ama kutoa mimba ndani ya muda huu kwa kuchelea uzito katika kuwalea watoto, kuchelea kushindwa majukumu mbalimbali ya maisha yao, kuwasomesha, kwa ajili ya maisha yao ya mbele au kutosheka na wale watoto ambao wanandoa tayari wameshapata, hapo itakuwa haifai.

3 – Haijuzu kuiporomosha mimba ikiwa tayari ni pande la damu au kinofu cha nyama mpaka kamati ya matibabu ya kuaminika ithibitishe kwamba kuendelea kwake kuna ukhatari juu ya usalama wa mama yake kwa njia ya kwamba kuna khatari akafa ikiwa mimba hiyo itaendelea. Hapo itafaa kuiporomosha baada ya kujaribu kutumia njia zote juu ya kuepuka khatari hiyo.

4 – Baada ya awamu ya tatu na baada ya kutimiza miezi mine haifai kuiporomosha mpaka madaktari wote wataalamu na waaminifu wathibitishe ya kwamba kubaki kwa mtoto huyo ndani ya tumbo la mama yake kutasababisha kufa kwake. Hapo itakuwa baada ya kutumia njia zote kwa ajili ya kuokoa maisha yake. Imeruhusiwa kuliendea jambo la kuitoa mimba hii kwa sharti hizi kwa ajili ya kuepuka dhara kubwa zaidi na kwa ajili ya kufanya manufaa makubwa zaidi.

Baraza baada ya kuthibitisha yaliyotangulia wanawausia watu kumcha Allaah na kuthibitisha kwanza katika suala hili.

Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.”

Katika “ad-Dimaa’ at-Twabiy´iyyah lin-Nisaa’” ya muheshimiwa Shaykh Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn imetajwa kwamba:

“Lengo la kuiporomosha mimba ni kutoa kile kipomoko. Ikiwa kile kipomoko kimeshapuliziwa roho, bila ya shaka yoyote ni haramu kwa kuwa ni kuiua nafsi iliyoharamishwa pasi na haki. Kuiua nafsi iliyoharamishwa bila ya haki ni jambo lililoharamishwa kwa mujibu wa Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya waislamu.”[3]

Imaam Ibn-ul-Jawziy amesema katika “Ahkaam-un-Nisaa’”:

“Yalipokuwa malengo ya ndoa ni kutafuta mtoto na si kwa kila manii hupatikana mtoto, hivyo basi akipatikana yamefikiwa malengo. Mtu kukusudia kuiporomosha kunapingana na kusudio la hekima. Isipokuwa ikiwa kitendo hicho kimefanyika mwanzoni mwa ujauzito na kabla ya kupuliziwa roho, basi hapo mtu atapata dhambi kubwa. Kwa sababu hiyo inapanda kwenda kwenye ukamilifu na utimilifu. Ingawa hiyo dhambi yake inakuwa ndogo kuliko ile ambayo tayari imeshapuliziwa roho. Akikusudia kutoa kitu ambacho kimeshapuliziwa roho inakuwa ni kama kumuua muumini. Amesema (Ta´ala):

وَإِذَا الْمَوْءُودَةُ سُئِلَتْ بِأَيِّ ذَنبٍ قُتِلَتْ

“Pindi mtoto wa kike aliyezikwa hali akiwa yuhai atakapoulizwa: Kwa dhambi gani aliuliwa?”[4][5]

Kwa hivyo, ee dada wa Kiislamu, mche Allaah na wala usifanye dhambi kama hii kwa lengo lolote miongoni mwa malengo. Usidanganyike na madai yenye kupotosha na ufuataji kichwa mchunga usiyotegemea akili wala dini.

[1] 02:228

[2] (11/151).

[3] Uk. Uk. 60.

[4] Uk. 108-108

[5] 81:08-09

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 41-44
  • Imechapishwa: 30/10/2019