Sayansi ya tiba imethibitisha faida kubwa mfungaji kukata swawm kwa kutumia tende. Bali ´Allaamah Ibn-ul-Qayyim amefanya hivo kabla yao. Wamesema kwamba kule Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kufungua kwa tende tosa, tende za kawaida au maji ni mpango wa kiafya wa hali ya juu sana[1]. Hilo ni kwa sababu mfungaji hutumia kwa kawaida mchana wake mwingi mafuta ya mwili wake na hivyo kiwango cha sukari mwilini hushuka na khaswa mwishoni mwa mchana. Dalili yake ni kwamba mfungaji huhisi udhaifu na uvivu na hivyo kukata swawm kwa tende mwili unarudi kuwa mchangamfu, kwa sababu tumbo linaweza kumeng’enya haraka virutubisho vya sukari vilivyomo kwenye tende. Matokeo yake mwili hunufaika navyo katika muda mfupi zaidi, pamoja na yale yaliyo ndani ya tende ya manufaa makubwa na virutubisho vinavyohitajika na mwili. Hapa kuna manufaa mawili mengine:

1 – Tumbo halitaelemewa na vyakula vikubwa vya moto vinavyowekwa ghafla ndani yake baada ya mchana wa swawm. Bali chakula kinaingia hatua kwa hatua. Hilo linakuwa kwa kuanza kufuturu tende, kisha mtu anaswali Maghrib kisha baada ya hapo ndio anakula chakula bila ya israfu.

2 – Kutosheka na kufuturu tende kunampunguzia ulafi mfungaji na hivyo hawezi kujitupa kwenye chakula akila bila kutafuna wala kuhisi ladha yake[2], kwani hilo – licha ya kwamba pia ni kinyume cha Sunnah – humshughulisha na kufanya haraka kuhudhuria swalah ya Maghrib kwa mkusanyiko. Bali pengine akakosa swalah kabisa.

Ikiwa mfungaji hakupata tende, basi akate swawm kwa maji. Maji huzima moto wa tumbo na joto la swawm na pia hulisafisha, kama ilivyothibitishwa na tiba ya kisasa.

[1] Tazama “Zaad-ul-Ma’aad” (04/313).

[2] Tazama “al-Ghidhaa´ laad-Dawaa´” uk. 126.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Minhat-ul-´Allaam fiy Sharh Buluugh-il-Maraam (05/32-33)
  • Imechapishwa: 10/02/2025