Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

166 – Tunamini alama za Qiyaamah, kukiwemo kujitokeza kwa ad-Dajjaal na kushuka kwa ´Iysaa mwana wa Maryam (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutokea mbinguni.

MAELEZO

Alama za Qiyaamah ni zile alama zinazofahamisha kuwa kwake karibu. Allaah (Subhaanah) amesema:

فَهَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا السَّاعَةَ أَن تَأْتِيَهُم بَغْتَةً ۖ فَقَدْ جَاءَ أَشْرَاطُهَا ۚ فَأَنَّىٰ لَهُمْ إِذَا جَاءَتْهُمْ ذِكْرَاهُمْ

“Je, basi wanangojea nini isipokuwa Saa iwafikie ghafla? Na kwa hakika zimekwishakuja alama zake. Basi kutoka wapi kutawafaa kukumbuka kwao itakapowajia?”[1]

Kusema kwamba kitakuja ghafla maana yake ni kwamba hakuna anayejua wakati wake isipokuwa Allaah pekee:

ثَقُلَتْ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ لَا تَأْتِيكُمْ إِلَّا بَغْتَةً

”Ni nzito katika mbingu na ardhi. Haitokufikieni isipokuwa kwa ghafla.”[2]

Jibriyl alisema kumwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nieleze kuhusu Qiyaamah.” Akasema: “Muulizwaji si mjuzi kama asivyo vilevile muulizaji.” Akasema: “Nieleze kuhusu alama zake.” Akasema: “Kijakazi kumzaa bibi yake na utaona wachunga wanaenda miguu chini, uchi na mafukara wakishindana kujenga majumba marefu.”[3]

Wanazuoni wametaja kwamba alama za Qiyaamah zimegawanyika mafungu matatu:

1 – Alama ndogondogo. Hizi zimekwishatokea na zimepita

2 – Alama za katikati. Hizi bado zinaendelea, mfano wa yale yanayoendelea hii leo katika maendeleo ya viwanda na mawasiliano, uchimbaji wa mali chini ya ardhi, utandawazi – kana kwamba ulimwengu imekuwa ni kijiji kimoja, kukusanyika kwa mayahudi Palestina wakimsubiri ad-Dajjaal.

3 – Alama kubwakubwa. Baadhi yake ni kujitokeza kwa ad-Dajjaal, kushuka kwa ´Iysaa (´alayhis-Salaam), kujitokeza kwa Ya´juuj na Ma´juuj, kujitokeza kwa Mnyama na kuchomoza kwa jua upande wa magharibi. Wakati kutajitokeza moja katika alama hizi, basi zitafuatia zingine.

[1] 47:18

[2] 7:187

[3] Muslim (8).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 244-245
  • Imechapishwa: 29/04/2025