Kwa sababu ya kuwa na ufahamu wa kimakosa kuhusu mambo yasiyokuwa ya kawaida, wengine wasiokuwa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wameingia katika makosa mengi. Mu´tazilah na wengineo wanaotumia akili mpaka hii leo wanapinga karama. Baadhi yao wanapinga mpaka baadhi ya miujiza, kwa sababu eti ni mambo yasiyosapotiwa na akili. Watu hawa wanatanguliza akili zao kabla ya kila kitu.

Kundi la pili juu ya maudhui haya ni waabudia makaburi na Suufiyyah. Wamechupa mipaka katika kuthibitisha karama mpaka wakawathibitishia nazo mawalii wa shaytwaan. Wanawathibitishia karama ambao hawaswali wala hawafungi. Wanakusudia yale mambo yasiyokuwa ya kawaida ya kishaytwaan. Wengine wamechupa mipaka juu ya mawalii na wakawaabudu pamoja na Allaah. Hivo ndivo wanavofanya waabudia makaburi. Ukisoma “Twabaqaat-ul-Awliyaa” cha ash-Sha´raaniy, basi utaona mambo ya ajabu na masimulizi ya batili. Kwa mujibu wao walii ni yule ambaye hana haja tena ya kufanya ´ibaadah. Mtu, pasi na kujali vovyote atakavyofikia katika wema na ´ibaadah, haifikii wakati akaacha kufanya ´ibaadah. Si Malaika, wala mawalii wala Mitume. Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Naapa kwa Allaah! Nataraji mimi ndiye mjuzi na mwenye kumcha Allaah zaidi katika nyinyi.”[1]

Haya yanasemwa na kiumbe bora kabisa na mbora zaidi ambaye ametembea juu ya ardhi. Allaah (Ta´ala) alimwambia:

وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ

“… na mwabudu Mola wako mpaka ikufikie yakini.”[2]

Hakuna yeyote aliyefikia ile nafasi aliyofikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), pamoja na hivyo kamwe hakupatapo kuacha kumwabudu Allaah. Allaah (´Azza wa Jall) amesema kumwambia Masiyh:

لَّن يَسْتَنكِفَ الْمَسِيحُ أَن يَكُونَ عَبْدًا لِّلَّـهِ وَلَا الْمَلَائِكَةُ الْمُقَرَّبُونَ ۚ وَمَن يَسْتَنكِفْ عَنْ عِبَادَتِهِ وَيَسْتَكْبِرْ فَسَيَحْشُرُهُمْ إِلَيْهِ جَمِيعًا فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فَيُوَفِّيهِمْ أُجُورَهُمْ وَيَزِيدُهُم مِّن فَضْلِهِ ۖ وَأَمَّا الَّذِينَ اسْتَنكَفُوا وَاسْتَكْبَرُوا فَيُعَذِّبُهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا وَلَا يَجِدُونَ لَهُم مِّن دُونِ اللَّـهِ وَلِيًّا وَلَا نَصِيرًا

”al-Masiyh kamwe hatojiona bora akate kuwa mja wa Allaah wala Malaika waliokurubishwa. Na yule mwenye kujiona bora akakataa kumwabudu na kufanya kiburi, basi atawakusanya wote Kwake. Ama kuhusu wale walioamini na wakafanya mema, basi atawalipa kwa ukamilifu ujira wao na atawazidishia katika fadhilah Zake. Ama kuhusu wale wenye kujiona bora wakagoma na kufanya kiburi, basi hao atawaadhibu adhabu iumizayo na wala hawatopata asiye Allaah mlinzi wala mwenye kunusuru.”[3]

Hii ni mada kubwa ambayo ni lazima kuijua, khaswa katika kipindi cha ujinga na mambo ya ukhurafi.

[1] al-Bukhaariy (5063) na Muslim (1110).

[2] 15:99

[3] 4:172-173

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 242-243
  • Imechapishwa: 29/04/2025