Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

165 – Tunaamini zile karama zilizopokelewa kutoka kwao na zikasihi kupitia wapokezi wenye kuaminika.

MAELEZO

Karama za mawalii ni mada kubwa. Karama ni yale mambo yasiyokuwa ya kawaida. Kama yamefanywa na Mtume, basi huyo ni miujiza. Kwa mfano miujiza ya Qur-aan, kwa sababu watu na majini wameshindwa kuleta kitu mfano wake. Isitose Qur-aan ndio miujiza kubwa kabisa. Miujiza mingine ni fimbo ya Muusa na zile alama tisa. Miujiza mingine ni kule ´Iysaa bin Maryam kuwahuisha wafu. Na ikiwa mambo haya yasiyokuwa ya kawaida yamefanywa na mja mwema, basi ni karama kutoka kwa Allaah ameipitisha kwake. Karama hiyo si yenye kutoka kwa mtu huyo. Mfano wa karama ni yale yaliyopitika kwa watu wa pangoni. Mfano mwingine ni matunda ya Maryam:

كُلَّمَا دَخَلَ عَلَيْهَا زَكَرِيَّا الْمِحْرَابَ وَجَدَ عِندَهَا رِزْقًا

”Kila Zakariyyaa alipoingia kwake katika chumba cha kuswalia basi alikuta kwake vyakula.”[1]

Riziki ilikuwa ikimjia wakati anamwabudu Allaah na hakutoka katika mihrab. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) ametaja katika kitabu chake “al-Furqaan” karama za watu katika ummah huu.

Lakini ikiwa mambo haya yasiyokuwa ya kawaida yatafanywa na kuhani au mchawi, basi ni jambo la kishaytwaan kwa lengo la majaribio na mtihani. Anaweza kuruka angani au akatembea juu ya maji. Akafanya mambo mbalimbali yasiyokuwa ya kawaida ilihali ukweli wa mambo ni katika matendo ya kishaytwaan.

Kigezo ni kwamba tunatakiwa kuyatazama matendo ya mtu. Ikiwa matendo yake yanaafikiana na Uislamu, basi yale anayoyafanya ni karama. Vinginevyo ni katika huduma wanazomfanyia mashaytwaan. Amesema (Ta´alaa):

وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا يَا مَعْشَرَ الْجِنِّ قَدِ اسْتَكْثَرْتُم مِّنَ الْإِنسِ ۖ وَقَالَ أَوْلِيَاؤُهُم مِّنَ الْإِنسِ رَبَّنَا اسْتَمْتَعَ بَعْضُنَا بِبَعْضٍ وَبَلَغْنَا أَجَلَنَا الَّذِي أَجَّلْتَ لَنَا ۚ قَالَ النَّارُ مَثْوَاكُمْ خَالِدِينَ فِيهَا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ ۗ إِنَّ رَبَّكَ حَكِيمٌ عَلِيمٌ وَكَذَٰلِكَ نُوَلِّي بَعْضَ الظَّالِمِينَ بَعْضًا بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ

“Na Siku atakapowakusanya wote: “Enyi hadhara ya majini! Kwa hakika mmewapoteza wanadamu wengi sana.” Na watasema marafiki zao wandani katika wanadamu: “Mola wetu! Tulinufaishana sisi kwa sisi na sasa tumefikia muda wetu ambao umetupangia.” Atasema: “Moto ndio makazi yenu – mtadumu humo, isipokuwa atakavyo Allaah. Hakika Mola wako ni Mwenye hekima wa yote, Mjuzi wa kila kitu. Na hivyo ndivyo Tunavyowafanya madhalimu kuwa marafiki wandani wao kwa wao kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.”[2] 

Majini wanaburudika kwa watu kwa njia ya kwamba wanawanyenyekea na kuwatii, watu pia wanaburudika kwa majini kwa njia ya kwamba wanawahudumia na kuwatekelezea matakwa yao. Kwa hiyo haya ni mambo yasiyokuwa ya kawaida ya kishaytwaan. Tofauti kati ya mambo hayo na karama inapatikana katika imani na matendo mema. Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

[1] 3:37

[2] 6:128-129

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 241-242
  • Imechapishwa: 29/04/2025